Na. Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel Tanzania Plc, imeilipa Serikali ya Tanzania, shilingi 32.9 bilion kama gawio na mchango maalum wa maendeleo baada ya kupata faida katika Mwaka wa Fedha 2019/20.
Mfano wa Hundi mbili za fedha hizo Fedha hizo ziliwasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Airtel Tanzania Plc, Bw. Gabriel Malata na kupokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ndiye mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James, Jijini Dodoma.
Akikadidhi hundi hiyo, Bw. Malata alisema katika kiwango hicho cha shilingi bilioni 32.99, shilingi bilioni 18.99 ni gawio na shilingi bilioni 14 ni mchango maalum wa maendeleo kwa Serikali baada ya Kampuni hiyo kupata faida ya bilioni 38.5 kwa mwaka unaoishia Disemba 2019/2020.
Akielezea mafanikio yaliyosababisha Kampuni yake kutoa gawio nono na michango ya maendeleo ya shilingi bilioni 1 kila mwezi, Bw. Gabriel Malata alisema licha ya uwekezaji mzuri katika upanuzi wa mtandao, idadi ya wateja imeongezeka kutoka milioni 11.4 Machi 2019 mpaka 13.3 milioni Machi 2020 na kwa sasa umiliki wa soko ni asilimia 27 kwa taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Aliongeza kuwa Airtel Tanzania Plc imetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 500 huku wanafanyakazi wa kigeni wakiwa saba tu na kupitia kampuni hiyo, Watanzania 350,000 wamejiajiri kwa kuuza huduma za kampuni ya Airtel Tanzania Plc kama vile kuuza vocha, mawakala wa Airtel Money hivyo kuchangia maendeleo ya uchumi kwa kulipa ushuru kwa Serikali
Na kwa kuunga mkono maendeleo ya serikali kama elimu na afya, Airtel pia imetoa 2.3 bilioni kwenye ujenzi wa Hosptili mkoani Dodoma na kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (VETA) kuzindua elimu kwa mtandao kupitia applikesheni ya VSOMO ambapo wanafunzi zaidi ya 500 wamehitimu.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James alisema tukio hilo la Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel kutoa gawio na mchango wa maendeleo wa shilingi bilioni 32.99 ni la kihistoria baada ya Serikali na Kampuni hiyo kuingia makubaliano maalumu ya kiutendaji na kiumiliki yaliyofanyika mwaka 2019.
“Baada ya majadiliano makali nay a muda mrefu, hatimaye Kampuni ya Bharti Airtel ilikubali kuongeza hisa za Serikali kutoka asilimia 40 hadi asilimia 49 na Bartel imebakiwa na asilimia 51” alifafanua Bw. James.
Aliipongeza Kampuni ya Airetl Tanzania kwa kutoa kiasi hicho kikubwa cha gawio cha cha shilingi bilioni 18.99 na kiasi kingine cha shilingi bilioni 14 zinazotokana na mchango wa Kampuni hiyo kwa Serikali ambapo inatoa shilingi bilioni 1 kila mwezi kuanzia mwaka jana na itakuwa ikifanya hivyo katika kipindi cha miaka mitano ambapo jumla ya shilingi bilioni 60 zinatarajiwa kupatikana.
Bw. James alizitaka Kampuni na Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa kuiga mfano wa Kampuni ya Airtel ili fedha zinazopatikana zichangie shughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi ikiwemo kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kuboresha huduma za jamii kama vile afya, elimu na maji kwa Watanzania wote.
“Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo bado zinatoa gawio dogo na zile ambazo hazitoi gawio, zinatakiwa kujitathmini na kuhakikisha zinafanya vizuri na kulipa gawio ili kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo”, alisisitiza Bw. James
Naye Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka alisema ofisi yake imeendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha Taasisi, Mashirika ya Umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa zinaendeshwa kwa tija na zinaendelea kutoa gawio endelevu kwa Serikali.
Awali, Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka aliipongeza Airtel Tanzania Plc kwa gawio na mchango wake wa maendeleo na kuitaka kuendelea kudhibiti matumizi na kuimarisha teknolojia katika utoaji wa huduma.
Aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni zote ambazo Serikali ni mwanahisa na kwamba wasiridhike na gawio walilotia bali mwakani watoe kiwango kikubwa zaidi kwa maendeleo ya nchi.
Alisema zaidi ya ufanisi wa kimapato, ofisi ya msajili inaendelea kufanya marekebisho katika mashirika na taasisi zilizo chini yake ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato.