Shule ya Awali na Msingi ya Taasisi ya Kiislamu ya Istiqaama iliyopo mkoani Tabora imeungua moto usiku wa kuamkia leo na kuteketeza baadhi ya vitu vya wanafunzi katika bweni moja.
Kikosi cha Jeshi la Zimamoto kikifanya jitihada za kudhibiti moto kwenye shule ya Awali na Msingi ya Istiqaama
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa amethibitisha kutokea kwa tukio la kuungua kwa moto kwa shule ya msingi.
Akizungumza na EATV / Radio Digital hii leo Septemba 27, 2020 Kamanda Mwakalukwa amesema kuwa moto huo ambao chanzo chake hakijajulikana haukusababisha madhara yoyote kwa binadamu.
''Ni kweli shule imeungua moto, hakuna madhara yoyote kwa binadamu lakini kuna bweni moja ambalo walikuwa wanakaa wasichana 45 vitu vyao vimeungua moto,” amesema RPC Mwakalukwa
Aidha Kamanda Mwakalukwa amesema kuwa uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea ili kubaini chanzo cha moto huo.