GARI lililowabeba baadhi ya maofisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kupata ajali katika eneo la Msoka, Kata ya Ngogwa, iliyopo kwenye Jimbo la Msalala, Shinyanga ni kupasuka kwa matairi mawili ya gari.
Gari hilo lililokuwa kwenye msafara wa Salum Mwalimu, mgombea mwenza wa Tundu Lissu (Chadema) lililowabeba maofisa wanne wa chama hicho, lilianguka na kuharibika vibaya jana tarehe 21 Septemba 2020. Hata hivyo, hakuna aliyefariki dunia.
Akizungumza leo tarehe 22 Septemba 2020, Gerva Lyenda, Katibu wa Salum amesema, chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa matairi ya gari ya upande wa kulia.
Amesema, gari hilo halikuwa mwendo wa kasi, na kwamba watu wote waliokuwamo katika gari hilo wametoka salama.
“Tairi la nyuma ilipasuka na la mbele likafuatia kupasuka. Zote za upande wa kulia, gari halikuwa mwendokasi, tulikuwa wanne ndani lakini hatujaumia, tulitoka salama,” amesema Lyenda.
Ameongeza, asubuhi ya leo wapo kwenye maandalizi ya kwenda hospitali kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya, kisha jioni wanaendelea na kampeni.
“Hatujajua kama tumeathirika kwa ndani. Tunajiandaa kwenda hospital ili kufanya vipimo vya afya,” amesema Lyenda bila kutaja jina la hospitali wanayotarajia kwenda.
Ajali hiyo ilitokea majira ya jioni wakati msafara wa Mwalimu ukitoka kwenye mkutano wa kampeni katika Jimbo la Msalala, wakielekea kwenye mkutano mwingine wa kampeni wilayani Kahama.