JESHI la Polisi kupitia kitengo cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya linawashikiria watu sita akiwemo raia wa Marekani Anderson Glenn (61) kwa tuhuma za kukutwa na kg. 51 za dawa za kulevya aina ya Heroine.
Pia watu hao wanadaiwa kukutwa na pipi 68, kifurushi kidogo cha gramu 10 na fedha Sh. 58,020,000 (milioni hamsini na mbili na elfu ishirini).
Akizungunza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya ACP Kabaleke Hassani amewataja watanzania hao kuwa ni, Said Mfaume, Mukrim Michael (48), mkazi wa Mbezi beach, Amini Sekibo (25), Salim Jongo (Jongo) na Tatu Nassoro (48) ambaye ni mama ntilie anayeishi Temeke Vetenary.
Akizungumza namna dawa hizo zilivyokamatwa ACP Hassan amesema, Septemba 2, 2020 mchana katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Karume Zanzibar Glenn alikamatwa akiwa na kg 04 za Heroine ambapo baada ya kuhojiwa polisi walibaini kuwa dawa hizo alipokea kutoka kwa Mfaume.
Amesema, juhudi zilifanyika na Septemba 3,2020 mtuhumiwa Mfaume alikamatwa ambapo katika mahojiano alikiri kuwa yeye ndio amesafirisha dawa hizo kutoka Tanzania bara na kumpatia Glenn ili azisafirishe kwenda Ubelgiji.
Kufuatia hayo, polisi walichunguza zaidi na kugundua kuwa dawa hizo zinamilikiwa na Michael na ndipo Septemba 6 Naye alikakamtwa na alipohojiwa alikiri kumkabidhi Mfaume dawa hizo na kuwaongoza hadi mahali alipoficha dawa kwa mtuhumiwa mwenzao Jongo.
Septemba 7, 2020 Jongo nae alikamatwa na alipohojiwa alikiri kuhamisha dawa hizo za kulevya na ndipo akawaongoza polisi hadi nyumbani kwa Tatu ambaye ni mama Ntilie.
Katika upanuzi zilipatikana dawa za kulevya aina ya Heroine kg 51 , pipi 68, kifurushi kidogo cha gramu 10 na fedha Sh. 58,020,000.
Jeshi la polisi linatoa onyo kwa wale wote wanaoendelea na biashara haramu ya dawa za kulevya kuacha mara moja kufanya hivyo, tutaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatia za kisheria.