Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori Nchini (TAWA) imeanza kutekeleza agizo la Rais la kuanzisha utaratibu wa kuuza nyama za wanyamapori kwenye Bucha zilizo chini ya Mamlaka hiyo ili kutoa fursa kwa kila Mwananchi aweze ya kutumia kitoweo hicho.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Kamishina wa usimamizi wa Wanyamapori Tanzania -TAWA Mabula Nyanda amesema licha ya kutekeleza agizo la Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli la kuanzisha Bucha za Nyamapori,ambazo zitatoa fursa kwa Watanzania ya kujipatia kipato na kuongeza fedha za kigeni.
Hata hivyo ameendelea kusema kuwa katika kurudisha faida kwa wananchi TAWA imeanzisha miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa ufugaji nyuki ambao unazalisha tani 1000 za asali na zaidi ya vikundi 58 na wanachama 268 wamenufaika na mradi huo.
Katika hatua nyingine amesema ili kupunguza uvamizi unaofanywa na wanyamapori katika maeneo ya makazi na mshamba hapa nchini,amewashauri Wananchi kuishi katika maeneo yaliorasimishwa kwa makazi ili kujilinda na wanyama wakali na waharibifu wanaotoka katika mbuga za wanyama na hifadhi za Taifa.
Hata hivyo amesema wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuthamini, kulinda na kudhibiti ujangili wa wanyamapori walio karibu na maeneo yao, ambapo mpaka sasa club 163 zimeanzishwa katika shule za msingi kwa lengo la kuwapatia elimu namna ya kuweza kuepukana na wanyama wakali na waharibifu.