*Vipindi vilivyorusha matusi ni The Switch na Mashamsha
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesitisha utoaji wa huduma kwa kituo cha Wasafi FM kwa muda wa siku saba kuanzia Septemba 12 mpaka Septemba 18 mwaka huu na siku ya leo wanatakiwa kuomba radhi kwa watanzania huku adhabu yao ikianza kesho.
Pia imekitaka kituo hicho kuomba radhi kwa umma wa Tanzania kwa kukiuka kanuni za utangazaji kupitia vipindi vya "The Switch na Mashamsham".
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema Agosti 4 mwaka huu kati ya saa 8 hadi 11 jioni na Agosti Mosi mwaka huu kati ya saa 4 na 6 mchana kupitia vipindi "The Switch na Mashamsham" walirusha maudhui yaliyotumia lugha yenye matusi na isiyokuwa na staha kwa jamii.
Amesema katika vipindi tajwa mtoa huduma alikiuka kanuni mbalimbali za utoaji huduma.
"Mtoa huduma ya maudhui anapaswa kufuata sheria Kanuni na masharti ya leseni sambamba na maelekezo yanayotolewa na TCRA katika utangazaji wa maudhui yake.
Amesema Septemba 10 mwaka huu TCRA ilitoa amri kwa kituo hicho ikiwataka kufika Septemba 11 mwaka huu kutoa maelezo kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yao kwa kukiuka kanuni za Mawasiliano ya kieletroniki na posta.
Aidha Mhandisi Kilaba alitoa rai kwa vyombo vya utangazaji vyote na watangazaji kuzingatia kanuni zote za utangazaji kwa lengo la kulinda maslahi mapana ya nchi na kimaadili.
Pia Baraza la Habari Tanzania (MCT) kutumia chombo hicho katika kuonya pale panapotokea utovu wa nidhamu au ukiukwaji wa maadili ya uandishi na utangazaji wa Habari.
Mhandisi Kilaba ameshindwa kunukuu matusi ya watangazaji kwa kudai ni kinyume cha maadili ya watanzania na ni ukiukaji wa leseni.