Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, limekiri kupokea taarifa za wizi mpya uliojitokeza wa pikipiki katika maeneo ya Tandika wilayani Temeke huku likiweka wazi hatua wanazozichukua kukabiliana na matukio kama hayo.
Akiongea na kipindi cha Drive cha East Africa Radio kinachoruka kila siku za Jumatatu mpaka Ijumaa kuanzia saa 10 jioni mpaka saa 2 usiku, John Richard ambaye ni mpelelezi kituo cha Polisi Chang'ombe amesema kuwa ni kweli wamepokea shauri la mwananchi mmoja alietambulika kwa jina la Juma Omary ambaye ameripoti kuibiwa pikipiki yake na watu wasiojulikana usiku wa saa tisa.
“Hilo shauri lipo kwangu na hata juzi nimejaribu kumpigia akaniambia ameumizwa sana na leo nimezungumza naye, nimemuambia akapumzike na kesho tuonane,upelelezi bado unaendelea", amesema Richard.
Kwa upande wake muhanga wa tukio hilo, Juma Omary ameelezea jinsi tukilo hilo lilivyotokea,na kusema "ilikuwa saa9 usiku nikitokea maeneo ninayopaki nikapakia abiria wawili wakike na wakiume ndipo pikipiki nyingine ikaja ubavuni mwetu na kutusukuma, tukadondoka na kutuvamia Ila abiria wangu walifanikiwa kukimbia .
Anaendelea “Juzi nilipata abiria saa 9:00 usiku, nikawapeleka mpaka eneo la Kaburi Moja Tandika, kuna pikipiki ikanisukuma nikaanguka, mmoja akatoa panga akanipiga kichwani, wakachukua pikipiki wakaondoka abiria walifanikiwa kukimbia, Kesi yangu ipo kituo cha polisi Chang'ombe na matibabu nimepata, nina majeraha kichwani nimeshonwa nyuzi tatu na mkononi nyuzi mbili, nashukuru sungusungu walikuwa msaada mkubwa maana ningekufa".