Rais Donald Trump ameahidi kumteuwa mwanamke wiki ijayo kujaza nafasi iliyowachwa wazi kufuatia kifo cha Jaji Ruth Bader Ginsburg, na kulishinikiza baraza la Seneti linalodhibitiwa na Warepublican kuidhinisha jina hilo bila kuchelewa.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni jimboni North Carolina, Trump alisema atamteuwa mrithi wa Ginsburg licha ya kupingwa na Wademocrat akiongeza kuwa kwa sasa hajui ni nani atakayemteuwa.
Wajumbe wa Republican wanataka mrithi wa Jaji Ginsburg apatikane kabla ya uchaguzi, huku Wademocrat wakisisitiza kuwa uamuzi huo utafanywa na rais atakayechaguliwa Novemba 3.
Mapambano yanayotarajiwa kuhusu kiti hicho kilichowachwa wazi, lini kitafutiwe mrithi na nani atakayekikalia, yanaugubika mkondo wa mwisho wa kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais kwa taifa ambalo tayari linakabiliwa na hali ngumu kutokana na janga la corona lililowauwa karibu watu 200,000, kuwaacha mamilioni bila kazi na kuongeza mivutano ya vyama na hasira.