MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema amestushwa na kupata wasiwasi juu ya kitendo cha wakurugenzi watendaji wa halmashauri nchi nzima kuitwa jijini Dodoma na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Dk. John Magufuli.
Amesema wakurugenzi watendaji wa halmashauri kwa mujibu wa sheria ndio wasimamizi wa uchaguzi hivyo kitendo cha kuitwa na Dk. Magufuli kimempa wasiwasi kwamba wanakwenda kupewa maelekezo ambayo yanaweza kufanana na kuleta matokeo yaliyotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019.
Akizungumza na wandishi wa habari jana katika ukumbi wa Nyakahoja unaomilikiwa na Kanisa Katoliki, Lissu alimtahadhirisha Dk. Magufuli kwamba kama anataka kujiweka katika mazingira magumu atoe maelekezo kwa wakurugenzi hao juu ya uchaguzi wa mwaka huu huku akisisitiza kwamba ana asilimia 100 kupata kila kitu kitakachozungumzwa kikao hicho.
“Mwaka jana Dk. Magufuli aliwaita Ikulu watendaji wa kata na vijiji nchi nzima na akatoa maelekezo ambayo kila mtanzania anajua kilichotokea katika serikali za mitaa kwa wagombea wa vyama vya upinzani kuondolewa, siyo kwamba tumelisahahu hilo, sasa yeye atoe maelekezo na litalotokea litakuwa juu ya kichwa cha Magufuli.
“Kama anataka nchi hii ivuruguke achezee uchaguzi wa mwaka huu, kama anasema hataki kutembea kwenda mataifa makubwa basi ajue atatembezwa na sheria kwenda huko kujibu mashitaka, haiwezekani katikati ya kampeni anawaita wakurugenzi, yeye ni mgombea kwa nini akutane na wale ambao wana mamlaka ya usimamizi wa uchaguzi,”alihoji Lissu.
MABANGO-TRA
Akizungumzia juu ya wagombea wa Chadema kutokuwa na mabango mengi kama ilivyo kwa CCM, alisema walipewa masharti na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba wanapaswa kuyalipia na endapo watachapisha mabango yenye gharama ya Sh milioni 10 wanapaswa kulipia Sh milioni 20 kitendo ambacho hawakubaliani nacho kwa sababu siyo ya biashara.
Lissu alisema licha ya kuwa na hali mbaya ya kiuchumi lakini Chadema inatarajia kupata fedhaa hivi karibuni ambapo wamejiandaa kutengeneza mabango makubwa ya wagombea akiwamo yeye na kuyabandika nchi nzima huku akibainisha kwamba hawatayalipia TRA.
“Hatuna fedha ya kuchezea kwa sababu vyuma vimekaza kweli kweli, fedha iliyopo ndio inatusaidia katika kampeni lakini nasema wazi kwamba inawezekana tukapata fedha kwa awamu ya tatu ya kampeni zetu, tumejiandaa kutengeneza mabango makubwa na madogo ya kuyabandika nchi nzima na hatutalipa hata senti moja TRA, nasema mabango hayo hayatabanduliwa na tusichezeana, kwanza nimepata taarifa CCM hawajalipia hayo mabango yao,”alisema.
ASIMULIA ALIVYOPIGWA MAWE
Lissu alisema katika kampeni yake ya awamu ya pili amekumbana na matukio matatu kuanzia Mkoa wa Kigoma, Kagera na Geita ambayo hayakumfurahisha sana huku akilipongeza jeshi la polisi kwa kazi kubwa waliyofanya na kuimarisha usalama wake kuanzia kwenye msafara barabarani na mikutano yake.
Alisema akiwa mkoani Kagera walishambuliwa na mawe na wafuasi wa CCM waliokuwa juu ya ghorofa la ofisi ya chama hicho wakati wanapita chini kitendo kilicholeta taharuki licha ya polisi kudhibiti vurugu hizo na kurejesha usalama.
“Tukio hilo limeleta doa katika kampeni hizo, na hii imetokana na CCM kuwa na hasira baada ya kuona watu wamejitokeza wengi ukizingatia alipopita Dk.Magufuli ilidaiwa walimzomea, tukio la pili nilipokuwa Geita Mjini tulikuta vijana wakiwa na mabango wameziba barabara na walitaka kuleta fujo lakini tukawa wapole ndipo walipoanza tena kurusha mawe, bahati nzuri polisi waliweza kutumia mabomu ya machozi na kuwakamata baadhi.
“Walilinda mkutano wangu mpaka naondoka nipo salama, tukio la tatu ni ambalo hata mimi sikutegemea ni kupata watu wengi sana kuanzia Mkoa wa Kigoma, Kagera, Geita na Mwanza yaani mpaka nafarijika moyoni, ndio maana napata nguvu ya kufanya mikutano kati ya 5 hadi 8 kwa siku ambapo kwa siku tatu ninakuwa na mikutano 20.
“Nilitaka kufanya mikutano hiyo kwa helkopita lakini tumeambiwa rubani wetu ana zaidi ya miaka 55 hivyo ni mzee, kikubwa nashukuru watanzania hasa wa Kanda ya Ziwa kuniunga mkono,”alisema Tussu na kuendelea kulipongeza jeshi la polisi.
POLISI WAMENITENDEA HAKI
Kuhusu jeshi la polisi, alisema vimemtendea haki katika kampeni hasa awamu ya pili, jambo ambalo hakulirajia kabisa huku akidai kuwa anasikitishwa na kitendo cha baadhi ya polisi kuhamishwa na kushushwa vyeo kutokana na kuimarisha usalama wake.
“Jeshi la polisi limebadilika sana na wamenipa ushirikiano wa hali ya juu kuanzia msafara na mikutano yangu, mtu kama mimi ambaye ni muathirika wa matukio ya polisi nimeshtushwa lakini maeneo ambayo nilipewa ushirikiano na polisi nimeambiwa wameondolewa na kuhamishwa, nimedokezwa kule Songwe, Geita, Kagera na Kigoma wamekumbana na hali hiyo, binafsi hadi sasa siwezi kuwasingizia jambo kwa namna walivyonilinda,”alisema.
MIKOPO
Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, alisema endapo atafanikiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atahakikisha anarejesha asilimia tatu ya mkopo kama ilivyokuwa awali wakati bodi ya mikopo inaanzishwa.
Alisema watu wasio na nia njema na Watanzania wameamua kupandisha asilimia ya mkopo kutoka tatu hadi 14 jambo ambalo linaleta ugumu wa kurejesha.
Pia alisema atahakikisha anaondoa ubaguzi uliopo sasa kati ya waliosoma binafsi na umma.
KUHUSU KUTUMWA NA MABEBERU
Hata hivyo alisisitiza kwamba kuna watu wachache wanasema ametumwa na mabeberu kugombea urais ambapo alifafanua kwamba Tanzania bila kushirikiana na mataifa yaliyoendelea haiwezi kupata maendeleo.
Alisema hao wanaoitwa mabeberu endapo wataamua kutoshirikiana na Tanzania ndani ya wiki moja watapata shida sana na kuwataka watanzania kuachana na propaganda hizo kwani miradi mikubwa nchini inafadhiliwa na mataifa makubwa.