Uagizaji Holela Wa Mayai Kutoka Nje Ya Nchi, Wazidi Kudhibitiwa



Na. Edward Kondela

Watanzania wametakiwa kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini yakiwemo mayai ya kuku ili kukuza sekta ya ufugaji ikiwemo ajira huku serikali ikisisitiza mayai ya kuku wa kienyeji na kisasa ubora wake unatokana na mchanganyiko wa vyakula anavyokula kuku. 


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro mara baada ya kutembelea shamba la ufugaji kuku wa mayai Afro Farm Limited lenye kuku elfu ishirini (20,000) wenye uwezo wa kuzalisha mayai zaidi ya makasha (trays) 500 kwa siku, na kubainisha kuwa serikali imedhibiti uagizaji holela wa mayai kutoka nje ya nchi na sasa mayai yapo mengi nchini.


“Udhibiti uingizaji holela wa mayai kutoka nje ya nchi soko sasa limepatikana na niseme udhibiti huo siyo nguvu ya soda ni kwamba ni suala endelevu na tutaendelea nalo na tunazidi kujipanga lakini sasa lazima tuhamasishe watanzania kwamba wapende vya kwetu, ni suala ambalo kama wizara tumejipanga mayai yanaleta afya bora na tunapoelekea uchumi wa viwanda tunahitaji watu wenye afya bora.” Amefafanua Prof. Gabriel.


Kuhusu wafanyabiashara wanaotozwa tozo ya shilingi elfu moja (1,000/=) kwa kila kasha moja la mayai (tray) kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar Prof. Gabriel amesema tayari kanuni zimeshabadilishwa na tozo imepungua hadi shilingi mia moja (100/=) kwa kasha moja na kusisitiza wadau wa sekta ya ufugaji kulipa kodi ili serikali iweze kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.


“Nitoe angalizo kwamba siyo vizuri sana mnapokuwa mnafikiria kuwa ifike mahali kwamba msilipe gharama yoyote kwa serikali, hilo hapana ni lazima mlipe kwa sababu mchango mnaotoa ndiyo unaojenga hospitali, barabara, shule n.k.” Amesisitiza Prof. Gabriel.


Aidha Katibu Mkuu Prof. Gabriel, ametoa wito kwa vijana kujiajiri katika sekta ya kuku kwa kuwa ni sekta ambayo ni rahisi na yenye mahitaji makubwa kwa watu kwa ajili ya nyama, mayai na mbolea huku akiwataka pia wafugaji wote watambue kwamba lazima waangalie mnyororo wa mapato, gharama na faida ili kupata kupata mafanikio makubwa na kuongeza ajira.


Pia amefafanua kuwa ni vyema wadau wa ufugaji wa kuku wa mayai kufuata kanuni bora za lishe ili waweze kuzalisha mayai bora badala ya kuwa na mayai mengi yasiyo na ubora na kubainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina kuku milioni 83 na mayai bilioni nne huku mahitaji ya mayai yakizidi kuongezeka ndani na nje ya nchi.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka pia wafugaji kutumia Dawati la Sekta Binafsi lililo chini ya wizara hiyo kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ya mitaji na miongozo kwa kuwa dawati hilo ni kiungo kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Afro Farm Limited Bw. Remen Kweka amewataka vijana kubadilisha fikra zao kwa kuhakikisha wanajifunza pindi miradi mbalimbali inavyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini ili kujiwekea mazingira ya kupata ajira na kubuni mitambo mbalimbali ya uzalishaji.


Bw. Kweka pia amewaasa wadau wa ufugaji wa kuku katika miradi mikubwa kutumia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupeleka sampuli za vyakula vya kuku ili kuhakikisha kuku wanakula vyakula bora ambavyo vitatoa matokeo chanya ya upatikanaji mayai yaliyo bora ambayo yanaweza kushindanishwa katika soko la kimataifa.


Bi. Amillen Kweka ambaye ni mke wa mkurugenzi wa shamba la Afro Farm amesema mradi huo umewawezesha kusomesha watoto shule pamoja na kuwasaidia akinamama kutokata tamaa na kuwafundisha juu ya ufugaji wa kuku wa mayai huku Bi. Emma Kweka ambaye ni mtoto wa familia hiyo akiwaasa vijana kuwa na shauku ya kujifunza ili kutafuta zaidi na kujiajiri kwa kuwa kujiajiri ni jambo zuri ambalo unaweza kupangilia jambo lako katika muda unaotaka na kusisitiza bidii na mipangilio ya kazi.


Shamba la ufugaji kuku wa mayai la Afro Farm Limited kwa sasa lina kuku elfu ishirini (20,000) na kuzalisha mayai makasha (trays) zaidi ya 500 kwa siku, huku likiwa na uwezo wa kuhifadhi kuku elfu arobaini (40,000) na linatumia mitambo ya kisasa katika kulishia kuku, kukusanya mayai pamoja na mbolea.



Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad