Umoja wa Ulaya Walaani Kunyongwa kwa Mwanamasumbwi wa Iran Navid Afkari
0
September 15, 2020
Umoja wa Ulaya imeungana na jamii ya kimataifa kulaani mauaji ya kikatili dhidi ya mwanamasumbwi wa Iran Navid Afkari. Umoja huo umesema adhabu hiyo ya kifo ni ya kikatili na isiyo ya kibinadamu na kuwa umoja huo unapinga mauaji ya aina hiyo.
Shirika la habari la Iran liliripoti kunyongwa kwa Afkari mnamo siku ya Jumamosi.Afkari, ambaye ni bingwa katika mchezo wa masumbwi alikuwa amehukumiwa kwa kosa la kumuua kwa kumdunga kisu mlinzi wakati wa maandamano ya kuipinga serikali mwaka 2018.
Shirika la habari la Iran limeripoti kuwa wizara ya mambo ya nje ya Iran leo Jumatatu imemuita balozi wa Ujerumani ili ajieleze juu ya ujumbe aliouandika katika mtandao wa Twitter wa kulaani mauaji ya Afkari.
Iran imesema ujumbe huo wa Twitter unachukuliwa kama kuingiliwa kwa mambo yake ya ndani.Marekani ambayo, tofauti na Umoja wa Ulaya pia inatekeleza adhabu ya kifo, pia imelaani kunyongwa kwa Afkari.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amelitaja tukio hilo kama shambulio dhidi ya ubinadamu.
Tags