UONGOZI wa simba umesema kuwa taarifa zinazoenea mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari zikieleza kuwa mchezaji wao nyota Meddie Kagere amepigana na Kocha Mkuu Sven Vandenbroeck sio za kweli.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa Simba Haji Manara amesema kuwa kumekuwa na taarifa ambazo zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa Kagere na Sven wamepigana jambo ambalo ni la kupikwa.
"Kwetu sisi Simba ni furaha siku zote na mambo hayo yalikuwa kitambo sio sasa kila kitu kinakwenda sawa hakuna ukweli wowote kuhusu Kagere kupigana na Sven.
"Huo ni uogo na umepikwa kusudi na kwa nia ovu ya kutuvuruga kwa kuwa mambo ndani ya Simba ni shwari hivyo tumeshajua na hatupo tayari kuvurugwa.
"Ili kujua kwamba taarifa hizo ni za uongo zinaelza kwamba Kagere alipigana na kocha mazoezini, jana Simba hawajafanya mazoezi na wachezaji walilala baada ya kocha kusema kuwa wachezaji wamechoka kwa kuwa walisafiri kutoka Arusha mpaka Mbeya, hivyo kama wamepigana mazoezini ni uwanja gani walifanya mazoezi?.
"Muda huu ndio wachezaji wanajiaandaa kwenda kuanza kufanya mazoezi, hatukubali na hatupo tayari kuvurugwa," amesema.
Simba ipo Mbeya ambapo iliwasili jana Septemba Mosi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Septemba 6, Uwanja wa Sokoine dhidi ya Ihefu FC.