OFISA Habari wa Simba SC, Haji Manara amesema Bodi ya Ligi (TPBL) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wameridhia maombi ya kushusha viingilio vya mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar.
Hata hivyo, baada ya Simba kusema hivyo gumzo kubwa limezuka kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya mashabiki wakiwakejeli kuwa wamepoteza mvuto.
Awali katika michezo ya Simba viingilio vilizoeleka kuwa ni 5000, lakini mpaka sasa timu hiyo imewasilisha maombi hayo ambayo huenda yatakuwa na tija kwa mashabiki wao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Manara, alisema kuwa tayari klabu hiyo imewasilisha maombi hayo kwa TPLB pamoja na TFF kwa ajili ya kupunguza viingilio hivyo kwa ajili ya kuleta hamasa kwa mashabiki wao.
“Tuna furaha wenzetu wa Bodi ya Ligi na TFF kuridhia maombi yetu ya kutaka mechi hizi za Dar es Salaam ili kuongeza hamasa zaidi kushusha viingilio hususani vya mzunguko, awali tulikubaliana kimsingi na Bodi ya Ligi na TFF kiingilio cha chini kitakua 3000 kutoka 5000.
“Taarifa rasmi ya aina ya viingilio na majukwaa yake kwa mchezo unaokuja tutatangaza kwenye kurasa zetu za Instagram za klabu lakini kwa sasa kiingilio cha chini ambacho tulitaka kishushwe zaidi kinaweza kuwa 2000 hadi 3000 na tutaridhika nacho,” alisema Manara.
Kikosi hicho cha mabingwa watetezi wa VPL, Simba kwa sasa kipo kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa raundi ya tatu dhidi ya Biashara United utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar saa 1:00 usiku na hapo ndiyo viingilio vipya vitatumika.