Wachezaji Kisinda, Carlinhos Hawakamatiki..Yaani ni Full Mzuka Yanga



UONGOZI wa Yanga upo katika hatua za mwisho kukamilisha kibali cha kocha wao, Mserbia, Zlatico Krmpotick na wachezaji wao wapya wa kigeni watakaokuwa sehemu ya kikosi chao kitakachocheza dhidi ya Tanzania Prisons.

Wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo ni Wakongo, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda ambaye tayari ameshaanza kuwa kipenzi cha Wanayanga, Carlos Fernandez ‘Carlinhos’, Michael Sarpong na Yacouba Songne pamoja na kocha wa makipa Vladimir Niyonkuru kutoka Burundi.

Yanga, keshokutwa Jumapili inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara 2020/21 utakaoanza saa 1:00 usiku.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema kuwa utaratibu wa kupata vibali vya wachezaji wao wapya wa kigeni na benchi la ufundi umekamilika kwa asilimia kubwa.

Bumbuli alisema wanategemea kuwatumia wachezaji hao katika mchezo wao wa ufunguzi wa ligi wakati timu hiyo itakapocheza dhidi ya Prisons, unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa.

Aliongeza kuwa timu yao inaendelea na mazoezi ya pamoja chini ya kocha wao, Zlatko katika kukiimarisha kikosi chao baada ya kukipokea kutoka kwa kocha msaidizi Riedoh Bardien, raia wa Afrika Kusini.

“Mashabiki wa Yanga waondoe hofu juu ya wachezaji wao wapya, kwani watakuwepo sehemu ya kikosi kitakachocheza mchezo wao wa kwanza wa ligi tutakaocheza na Prisons.

“Kikubwa wafahamu kuwa tumeshakamilisha taratibu zote za kupata vibali vya wachezaji wetu wa kigeni pamoja na benchi la ufundi kwa asilimia kubwa baada ya kufuata taratibu zote kutoka serikalini.

“Kwani tunafahamu umuhimu mkubwa wa mchezo huu ambao tunahitaji kupata pointi tatu muhimu zitakazotuongezea morali kupata matokeo mazuri kwenye michezo ijayo inayofuatia.

“Katibu wetu yupo mkoani Dodoma kwa ajili ya kumalizia mchakato huo wa vibali, kesho (jana) au keshokutwa (leo) atarudi kwa ajili ya kumalizia taratibu ambapo hadi itakapofika Jumamosi tutakuwa tumeshakamilisha,” alisema Bumbuli.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad