Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya DSM imewahukumu kunyongwa hadi kufa Watu watano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kumuua aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk.Sengondo Mvungi.
Hukumu hiyo inakuja ikiwa ni miaka 7 tangu watu hao wafikishwe kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Waliohukumiwa ni Msigwa Matonyaz, Mianda Saluwa, Paulo Mdondono, Longishu Losingo na John Mayunga.
Pia Mahakama hiyo imemuachia huru Juma Kang’ungu baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Seif Kulita ambapo upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mawakili, Credo Rugaju, Lilian Lwetabura, Veronica Mtafya.
Katika kesi hiyo Upande wa Mashitaka uliwasilisha mashahidi 16 na vielelezo 15.
Akitoa hukumu hiyo Jaji Kulita amesema ameridhika pasina kuacha shaka na ushahidi wa Upande wa Mashitaka, hivyo anawahukumu washitakiwa wote kunyongwa hadi kufa isipokuwa mshitakiwa wa Tano ambaye ni Juma Kang’ungu ambaye ushahidi wa mashitaka haumkumgusa.
Kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na washitakiwa hao kufikishwa ni Novemba 22, 2013.
Katika kesi ya msingi washtakiwa kwa pamoja walidaiwa kuwa Novemba 3 mwaka 2013 huko Mbezi Msakuzi Kiswegere walimuua kwa kukusudia Dk.Sengondo Mvungi.