Wanajeshi 10 wa Chad wameuawa walipokuwa wakizishambulia ngome za kundi la wanamgambo la Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad.
Katibu mkuu wa mkoa huo, Sadick Khatir, ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba wanajeshi saba pia walijeruhiwa katika uvamizi wa siku ya Alhamisi huku akithibitisha habari zilizotolewa na chanzo kimoja jeshini ambacho hakikutaka kutambulishwa.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi, Azem Mbermandoa, hakuthibitisha idadi hiyo ya vifo, lakini alisema kuwa jeshi la Chad limeharibu ngome ya wanamgambo hao wa Boko Haram na kuchukuwa silaha na risasi.
Kundi hilo la itikadi kali ambalo lilianza nchini Nigeria mnamo mwaka 2009, limeweka ngome katika visiwa vya Ziwa Chad, eneo kubwa la mabwawa kwenye mpaka kati ya Nigeria, Chad, Niger na Cameroon.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, linasema kuwa zaidi ya watu 360,000 wameyakimbia makaazi yao nchini humo ili kuepuka mashambulizi na pia mafuriko.