Wanajeshi wanne wa Cameroon wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kutokana na jukumu lao katika mauaji ya wanawake wawili na watoto wawili mwaka 2015.
Mauaji hayo yalinaswa kwenye kanda ya video ambayo ilisambazwa mitandaoni mwaka 2018 ikionesha jinsi wahasiriwa walivyofungwa macho na kupigwa risasi.
Serikali awali ilikana na kusema video hiyo ni ”taarifa ghushi ” lakini baadae ikawakamata wanajeshi saba.
Uchunguzi wa BBC Africa Eye ambao uliangazia kisa hicho ulionesha kilichotokea katika kijiji kimoja cha mbali kaskazini mwa Cameroon.
Pia iliwaonesha maafisa watatu waliotekeleza kitendo hicho.
Katika video hiyo, maafisa wanaonekana wakiwatuhumu wanawake hao kwa kujihusisha na Boko Haram, kundi la wanamgambo wa Kiislam ambalo mashambulio yake katika nchi jirani ya Nigeria yamesambaa na kuvuka mpaka.
Wahasiriwa hao miongoni mwao akiwemo mtoto mchanga aliyekuwa amefungwa mgongoni na mmoja wa wanawake hao, walitembezwa kwenye barabara ya vumbi kufungwa macho kwa kitambaa na kisha kupigwa risasi mara 22.
Saba kati ya wale walioshitakiwa katika mahakama ya kijeshi mji mkuu wa Yaoundé, waliondolewa mashitaka.
Mauaji ya wanajeshi wa Cameroon
Mafisa wanne walihukumiwa kifungo cha miaka kumi jela kwa kutekeleza mauaji ama kushirikiana kufanya uhalifu, huku afisa wa tano akipokea kifungo cha miaka miwili kwa kurekodi kanda ya video ya tukio hilo na kuisambaza.
Uchunguzi wa BBC ulifanya kisa hicho kuzua gumzo kimataifa huku baadhi ya watu wakielezea masikitiko yao kwenye mtandao wa Twitter. Taarifa hiyo iliwafikia mamilioni ya watazamaji mitandaoni.
Nchi ilipatwa na mshangao wakati video hiyo ilipotolewa mara ya kwanza 2018 lakini serikali ilipuuzilia mbali.
Awali, msemaji wa serikali alisema video hiyo ilirekodiwa nchini Mali na sare za kijeshi zilizooneshwa kwenye kanda hiyo sio zile zinazotumiwa na wanajeshi wa nchi hiyo katika eneo hilo la Cameroon.
Lakini ushahidi uliendelea kutolewa hali ambayo ilifanya kuwa vigumu kuficha.
Ni nadra sana kwa wanajeshi kufungwa kwa kuua raia nchini Cameroon lakini ishawahi kufanyika tena.
Maelezo ya video,Mauaji Cameroon: Waliyomuua mwanamke huyu wafichuliwa
Wanajeshi watatu kwa sasa wanahudumia kifungo jela kwa kuwaua watu 13 katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ambako majeshi yanakabiliana na makundi yanayotaka kujitenga.
Kifungo cha miaka 10 huenda kikaonekana adhabu ndogo lakini inaendana na visa kama hivyo, wakili mmoja ameiambia BBC.
Urefu wa kifungo huamuliwa na jaji, mazingira ya uhalifu uliofanywa na tafsiri yake ya sheria.