Wasanii Wanaokufa kwa Wimbo na Kufufuka
0
September 11, 2020
WIMBO mmoja haukeshi. Msanii hawezi kuishi kwenye sanaa miaka mingi kwa kutegemea ‘hiti’ moja aliyotoa. Maisha ya msanii ni kama pumzi unapovuta hewa safi. Ikiingia ndani ya mwili, inaharibika na kuwa hewa chafu, hivyo unahitaji kuitoa nje na kuvuta nyingine ili uendelee kuwa hai.
Kwa msanii kutoa ngoma kali leo, si kibali cha yeye kukaa kwenye piki milele; cha kukumbuka ni kwamba, ngoma ikiwafikia walaji, huchakaa kama mfano wa pumzi uliyoitoa. Diamond wa wimbo wa Mbagala alishachakaa; leo tunaye Mondi wa Jeje na Yope, mwaka ujao sijui tutakuwa na Mondi wa kali ipi?
Ni hakika Ali Kiba anayetamba hivi sasa na “Dodo” hawezi kubaki juu kisanii hadi mwakani kwa kukamata mitima ya mashabiki wake kwa wimbo huo. Lazima afanye kitu kipya kama kweli anataka kuendelea kuwa Ali Kiba, vinginevyo ajiandae kuitwa “Zilipendwa.”
Tunao akina ‘Zilipendwa’ wengi kwenye Muziki wa Bongo Fleva, inaweza kuwa vibaya kuwaita “wafu” lakini ni wazi kuwa kuna wasanii wengi hapa Bongo wamekufa kabisa kimuziki na kubaki historia. Peruzi dunia utaona wasanii na wanamuziki waliotamba zamani, leo hawasikiki; wamepotea na kupotelea mbali kabisa.
Nikukumbushe; kuna mwanamuziki mmoja wa DRC Kongo, aitwaye Kanda Bongo Man, enzi zake alikuwa moto wa kuotea mbali. Leo unapomsifu Diamond kufanya shoo ya kiingilio kikubwa, unakuwa umesahau kuwa Kanda Bongo Man aliwahi kuja Bongo mwaka 1992 na kupiga shoo yake ndani ya Uwanja wa Uhuru enzi hiyo ukiitwa Taifa, kwa kiingilio cha shilingi laki moja na watu walijaa uwanjani.
Kanda Bongo Man alikuwa “Man” kweli enzi hizo. Kwa miaka mitano 1990-1995 wimbo wake wa Isambe ulikuwa na kishindo cha ajabu.
Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, anamkumbuka Man jinsi alivyomponza pale alipoonekana kwenye vyombo vya habari akiwa amepiga naye picha, ambapo watu walimlaumu kwa kuendekeza starehe na kupuuzia mgomo wa madaktari uliokuwa ukisababisha wagonjwa kupoteza maisha.
Stori isiwe ndefu; hoja yangu ni kwamba, muziki ni pumzi ukiacha kuvuta hewa safi unakufa; ndivyo ilivyokuwa kwa Kanda Bongo Man kafa kimuziki.
Pitapita kwenye mitandao ya ng’ambo utaona pia kuna wasanii wengi wamekufa kimuziki, ukiambiwa huyu alikuwa mkali wa pini unasema: “Weeee!” Hakuna kazi ngumu kwenye sanaa kama “kuishi na sanaa” usikia wasanii wanalalamika “Oooh, muziki una stress” ujue wanalalamikia jambo hili.
Hiti mpya za kuwafanya wasife kisanii ni kiama cha wasanii wengi, maana msanii akizubaa tu kwenye hili, jamii inamzika akiwa hai. Ofa za bia, simu za washikaji mara moja zinakata, shoo zinayeyuka na heshima inashuka mjini, huku mema yake yakisahaulika haraka.
Hata hivyo ugumu wa msanii kuishi na sanaa unatofautiana kwa makundi mawili muhimu ya wasanii. Kundi la kwanza ni lile la “Mastaa” hawa maisha yao ya sanaa huwa hayafi haraka; wanasameheka na jamii pale wanapokuwa kimya kwa muda au kutoa ngoma mbovu baada ya kutamba na pini za kufa mtu mfululizo.
Harmonize, Ali Kiba, Mondi, Nandy, Nay wa Mitego, Zuchu na mastaa wengine, unaweza kuwaweka kwenye kundi hili la kwanza. Kwenye muziki ukikua sana utakufa taratibu, tofauti na wasanii wa kundi la pili, yaani wale “Mastaa wajao” wao kifo kiko nje nje, wakimisi kidogo tu, chali.
Msanii aliyebahatika kutoka kwa kuachia singo moja matata huwa ana kazi ngumu ya kubaki sokoni, kwani wimbo wake ukipoa kabla hajapakua mwingine, anakuwa marehemu wa muziki. Fasta watu wanammwaga na kuendelea na shughuli zao, jambo ambalo linawapa wakati mgumu kweli hawa ‘andagraundi’ wanaotaka kupiki kistaa.
Wakati naelekea mwisho wa makala haya, nimewaangazia wasanii watano Bongo, ambao siyo mastaa sana ila wamekuwa hodari “Kufa” na “Kufufuliwa” na ngoma zao.
Vigezo nilivyotumia ni kwamba wanajiendesha wenyewe, yaani hawana menejimenti madhubuti, hawana ‘fanibezi’ kubwa kwenye mitandao ya kijamii na hawana sapoti kubwa ya mashabiki mitaani, lakini wanaendelea kukomaa na gemu kibishibishi.
DULA MAKABILA
Jamaa ukimtathmini vibaya, unaweza kudhani ni kama yupoyupo tu kwenye sanaa lakini ni mbaya kinoma. Amekuwa mtundu sana wa kuwatekenya wamashabiki zake kwa ngoma zinazobamba kitaani; namaanisha Singeli mwanangu.
Kabla ya yote, hebu onja mashairi kiduchu ya wimbo wake wa HUJAULAMBA: Aah, siwezi kwenda na wewe, sababu hujaulamba, Yaani we bora utulie nyumbani, mwanangu hujaulamba Aah, Micheni wa dogo Ngote, mwanangu hujaulamba Jamani we bora utulie nyumbani, mwanangu hujaulamba.
Dulla nimetoka mbali, mpaka namiliki gari Lawama zako mimi sijali, kaulambe kama unataka safari. Makabila nimetoka mbali, mpaka namiliki gari…
Vipi hapo, ni kama utamu unakuja kwa kasi lakini ndiyo kazi ya mshikaji, mara zote akitoa hiti wanaomsubiria akwame amekuwa akiwa ‘prufu wrong’. Angalia ngoma zake kama Dua, Nitakuwaje, Ningekuwa Demu, zote ni kama jamaa alikuwa anavuta hewa safi ikichafuka kitaa anatema na kuachia utamu mwingine.
BEKA FLAVOUR
Nifanye nikuone kioo kwako nijitazame eh Nifunike kwa upendo kwingine nisione he Nifanye nijione me stronger kwako ni simame eh Nipepee kwa upendo pressure inishuke eh. Niweke kwenye sayari nzuri ya mapendo Niishi nikifurahi me na wewe Nionyeshe mapendo tena kwa vitendo Maneno yasituharibie…
Beka amekuwa msanii ambaye anatarajiwa kufa kisanii mara kadhaa lakini wapi; kifo kikija anakata rufaa anasavaivu. Mpe shavu tu kwa ngoma zake kama Sarafina, Kibenten, Tuwesare, hata kama humkubali kiivyooo!
ASLAY
Alianza kushaini na jina la Dogo Aslay akiwa Yamoto Bendi, lakini kwa sasa amekua, anawajua hadi wadada. Aslay amedumu kwenye gemu kwa muda mrefu, kitu kilichompa uhai ni hiti, kila akibandua anabandika nyingine kali kitaa kunanuka.
Wapo waliombeza wakasema “ameamua kuwa kivyake atapotea” lakini miaka imepita yupo kwenye gemu na utamu kama huu. Mhhhh iyee Yani raha hata tukilala na njaa Kila saa nakuona mpya mamy Tena raha huku ninavimba kitaa Unang’aa hata kwenye giza mamy Basi tulia eh, kama maji kwenye mtungi baby Nitakulea eh, ilimradi unipe heshima Kama mbolea eh, nitatia ili unawiri sana Nimekuzoea eh, ukiniacha itaniuma sana…
Haya ni sehemu ya mashairi ya wimbo wa Aslay wa Angekuwepo, lakini anazo pia hiti nyingine nyingi kama Usiitie Doa, Natamba, Muhudumu na Hauna, zilizomfanya aendelee kuishi kwenye akili za wapenda muziki Bongo.
MARIOO
Kuna wakati watu walikuwa wanadhani yupo kwenye Lebo ya Wasafi chini ya Mondi, kumbe dogo yuko kivyake. Amekuwa akitoa hiti anaonekana kama kabahatisha flani hivi lakini weeee!!!
Hebu cheki mikato hii: Dengula nyonga msokoto Maana mimi nimekuja na bapa Masha luv wee lete watoto Wanyonyonga party za kukata Nyumbani mimi nimechoka Mavitu ya mama Nataka dhuluma dhuluma eeh Nipate ndogo ndogo baridi mwanana…
Kitu hiki kinaitwa Wauwe na kiliwaua kweli mtaani, akina dada wengi walikuwa hawashikishiki kila kona unasikia Marioo. Huyu naye kwangu amekuwa msanii ambaye anajua kutoka na kuingia, akifa kwa wimbo anafufuka kwa wimbo; yaani bampa tu bampa.
Ukisikia songi linaitwa Unanikosha, Raha, Unanionea na Dar Kugumu, basi ujue mhusika ni Marioo, ambaye amejua kuishi na sanaa kwa muda mrefu.
MZEE WA BWAX
Kwenye muziki wa Singeli kuna vichwa vingi, lakini mimi hiki nakikubali. Dogo anajua kuishi na muziki kwa staili ya uswahilini.
We marota usione sikupigii Sijaweka salio Mwanangu usione nakudharau Sijaweka salio Mmmh baby wangu usione sikupigii Sijaweka salio Mchapu yangu usione nakudharau Sijaweka salio We masimu boti kisimu changu laini moja Nieke Tigo nieke Voda?
We masela kisimu changu laini moja Nieke Tigo nieke Voda? Hayo ni sehemu ya mashairi ya wimbo wa Kisimu Changu ambao kiuswazi dogo anakubalika balaa. Mzee wa Bwax amekuwa ni msanii anayechungulia tundu la mashabiki wake na kuwaletea wanachotaka; kifupi hapoi.
Ukichoka Kisimu Changu, sikiliza Salio, Unalinga Nini na Sanamu La Michelini, zote hizi ni hiti zinazomfanya bwa’mdogo asipotee kwenye gemu kirahisi.
Makala haya yanaishia hapa na kamwe yasichukuliwe kama kuwapa ufalme wasanii hawa, ila ni kutambua jinsi wanavyopambana. Huu ni mtazamo wangu kama na wewe unao wako na kuna msanii ambaye siyo mkubwa ila ameweza kushika gemu kibishibishi, hebu tupia mawazo yako kwa namba 0714-895 555.
MAKALA: MWANDISHI WETU
Tags