Waendesha mashtaka wa Uturuki wametoa waraka wa pili wa mashtaka dhidi ya raia sita wa Saudi Arabia kwa mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi raia wa Saudia yaliyofanyika mwaka 2018 katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul.
Shirika la habari la Anadolu limeripoti hii leo kuhusu uamuzi huo na kusema kwamba wawili kati ya watuhumiwa hao sita waliotajwa kwenye nyaraka zenye kurasa 41 za mashtaka hayo kutoka ofisi ya mwendesha mashtaka mjini Istanbul, ni pamoja na wafanyakazi wa ubalozi mdogo wa Saudi Arabia.
Kesi kuhusu mauaji ya Khashoggi ilifunguliwa kwa mara ya kwanza mwezi Julai mjini Istanbul na raia 20 wa Saudi Arabia walisomewa mashtaka bila ya kuwepo mahakamani.
Ripoti ya leo ya mwendesha mashtaka haikutaja ikiwa washukiwa hao sita ni miongoni mwa wale ambao tayari wameshashtakiwa mwanzoni.