Dar es Salaam. Mshambuliaji kinda Mtanzania, Amiri Salum anayeichezea klabu ya Karabuk Koyuspor SK na wadau wengine wa soka nchini Uturuki, wamemkaribisha kwa mikono miwili nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.
Samatta, ambaye ameichezea Aston Villa kwa miezi nane tangu ajiunge nayo akitokea KRC Genk ya Ubelgiji, ameonekana kutokuwa na nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kocha Dean Smith mbele ya Ollie Watkins aliyesajiliwa kutoka Brentford.
Amiri anayecheza soka la kulipwa Uturuki kwenye klabu ya Daraja la Tatu, alisema alizisikia taarifa za kutua kwa Samatta nchini humo tangu Jumatano, lakini imeonekana kuwa siri.
“Nina uhakika kuwa Samatta atakuwa mfalme mpya hapa kwa sababu uwezo wake ni mkubwa, kilichotokea Aston Villa kama amekichukulia kama sehemu ya changamoto anaweza kuwa bora zaidi hapa.
“Fenerbahçe ni klabu kubwa na mashabiki wake wameonekana kuwa na imani juu yake, wanamsubiri kwa hamu,” alisema Amiri.
Shaaban Mussa, ambaye ni Mtanzania anayesoma nchini Uturuki, alisema Samatta anatakiwa kujiandaa kisaikolojia na utata wa mchezo wa mahasimu, wakikutana huwa ni zaidi ya ‘derby’.
Nurdin Hussein, ambaye ni shabiki wa Fenerbahçe anayeishi Instanbul alisema: “Ni fahari kwetu kuona Mtanzania mwenzetu anakuja kutuwakilisha, nasubiri kwa hamu kumuona.”
Upande wake Simon Msuva ambaye anaichezea Difaa El Jadida ya Morocco, alisema anasubiri kuona mambo yakitangazwa rasmi lakini vyovyota itakavyokuwa ataendea kumsapoti.