Chama cha ACT Wazalendo leo Septemba Mosi,2020, kimezindua rasmi kampeni zake mkoani Lindi na kumnadi mgombea wake Urais kupitia chama hicho Bernard Membe huku kwa upande wake akitaja mambo mbalimbali yaliyomsukuma kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza na wananchi wa Lindi, Membe amesema kuwa miongoni mwa mambo yanayomuumiza ni pamoja na suala la ubovu wa barabara za Kusini na la pili ni dharau wanayofanyiwa watu wa Kusini.
"Linalonifanya nigombee ni dharau tunayofanyiwa, watu wa Kusini tunaonekana kama wajinga wajinga, malofa, hatuna akili, watukanwe Shangazi zetu sijui ni kwa utani au ni kwa dhihaka lakini ni dharau ambazo viongozi wa nchi hawapaswi kuwafanyia watu wa Kusini’’, amesema Membe.
Aidha wakati akiomba kura kwa wananchi Membe amesema kuwa, "Sisi ACT wazalendo tuna wateja wazuri ndani ya CCM sababu na wenyewe wamechoka na tuna makundi mawili, la kwanza ni lile lililoamua kuachana kabisa na CCM la pili linasema acha tubaki na kadi zetu lakini Oktoba 28 tutamchagua Membe"