Askofu mmoja wa kanisa la Kipentekoste huko Magharibi mwa Kenya, amewagawanya waumini wake, baada ya kuamua kumuoa mwanamke mmoja ambaye zamani alikuwa akifanya kazi ya ukahaba.
Hatua yake hiyo, imewafanya baadhi ya wahubiri wenzake waliokuwa wakimsaidia katika kanisa lake, kuamua kujitenga na kutoka na kiasi kikubwa cha waumini wake.
Askofu Joel Osoro amejuta kubaki peke yake na mke wake ‘mpya’ na watu wanaohesabika kwa ajili ya mapenzi yake kwa mwanamke huyo.
Yote yalianza wakati mwanamke huyo, raia wa Uganda ambaye alipofichua kanisani kwamba ameokoka na anataka kusamehewa dhambi zake, kwani alikuwa kahaba na kazi yake aliifanya kuanzia Kampala hadi Bukavu huko Mashariki ya DRC
Mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Celestione, alipoamua kuhamia mji wa Webuye, hakuna aliyejua kwamba uamuzi wake huo utatishia kulivunja kanisa ambalo lilikuwa limenawiri na kukita mizizi katika eneo hilo kwa takriban miaka 20.
Baadhi ya waumini walimuelezea mwanamke huyo kuwa alipohamia mji wa Webuye, wengi walimuona kama mgeni mpita njia ambaye baadaye angechoka na maisha ya polepole ya eneo hilo, kisha kurejea alikotoka, ila huo haukuwa mpango wake.
“Mwanzo alianza kuuza vitu katika soko la karibu na muda sio mrefu akawa mwenyeji na kutafuta kanisa la kuanza kuabudu. Jumapili kadhaa akaonekana kanisani, kumbe kamvutia mhubiri Osoro ambaye alianza kumpekuapekua ili kumjua ‘kondoo’ huyu mpya katika kanisa lake katokea wapi,” alisema muumini huyo.
Aidha, Celestine aliyasema yote na hakuficha kwamba, alikuwa akijutia maisha yake ya ukahaba ya hapo awali, lakini sasa alikuwa tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha yake.
Askofu Osoro, naye aliahidi kumsaidia katika safari yake mpya ya ukombozi.
Aidha, Osoro alipowatangazia waumini kwamba ameamua sasa kumuoa Celestine, wengi hawakuamini na wanawake katika kanisa hilo, hasa waliamini kwamba mwanamke huyo alikuwa ‘shetani’ ambaye katumwa kuja kumharibu mhubiri wao.
Waumini wengi walimpa Osoro chaguo la kuamua kati ya kumuoa Clestine au kuondoka kanisani.
Yeye ndiye aliyekuwa mwanzilishi na ‘Askofu mkuu’ wa kanisa hilo ambalo sasa lilikuwa na matawi kadhaa katika eneo la Magharibi.
Joto lilipanda na hatimaye baadhi ya wahubiri katika kanisa hilo waliamua kuondoka na waumini ili kuanzisha makanisa yao maeneo mengine baada ya Osoro kusisitiza kwamba, lazima Celestine awe mke wake.
Mwishowe, askofu huyo alioana na mwanamke huyo kwa lazima katika kanisa lililosalia na wafuasi wachache, huku laana na shutuma za waumini wake walioondoka, zikiendelea kuighubika ndoa yao changa.