Raia wawili wa China ambao walirejea katika makazi yao Januari, baada ya kuambukizwa virusi vya corona katika kipindi ambacho taifa hilo lilikuwa katikati ya kilele cha maambukizi ya virusi vya corona, wamehukumiwa kifungo kwa kushindwa kujiweka karantini au kushindwa kutoa taarifa.
Baada ya kurejea kutoka mjini Wuhan, watu hao walitembelea kwenye maduka makubwa na maeneo mengine ya wazi, huko mjini Yibin, jimboni Sichuan. Inaelezwa walikuwa huru kwa zaidi ya wiki moja kabla hawajaanza kuonesha dalili.
Mahakama imesema takriban watu 306 ambao walikutana na watuhumiwa hao walitengwa kwa uchunguzi ingawa hawakuonesha ishara ya kuambukizwa.
Watuhumiwa hao ambao walitajwa kwa jina moja moja akiwemo Deng, amehukumiwa miezi 11 na Tian miezi tisa na kwa mujibu wa mahakama vifungo vyao vimeahirishwa hadi baada ya miezi 18.