Waziri Simbachawene Aihakikishia Marekani Kuwa Nchi Ipo Salama Kwa Raia Na Wageni



Na Mwandishi Wetu MOHA-Dodoma
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ameihakikishia Marekani kuwa, Tanzania ipo salama na itaendelea kuwa salama kwa raia wake na wageni mbalimbali waliopo na wanaoingia nchini.

Akizungumza na Balozi mpya wa Marekani Nchini, Dkt Donald Wright, ofisini kwa Waziri huyo, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, jana, Simbachawene amesema usalama wa nchi upo juu na kwamba tumefanya vizuri katika kutambulisha wageni katika maeneo ya uwekezaji na utalii.

“Mheshimiwa Balozi nikuhakikishie tu, nchi yetu ipo salama sasa kuliko wakati mwingine wowote, na hatujawahi kuwa na kesi za ajabu, hii kutokana na uimara wa Serikali ya Rais Magufuli ambayo ipo wazi na imefanikiwa kudhibiti rushwa,” alisema Simbachawene.

Pia Waziri Simbachawene alisema Serikali inaendelea kudhibiti biashara haramu ya binadamu ambapo mpaka sasa imeweza kuwarudisha Wasomali 1,300,000 wanaopita nchini kwenda Afrika Kusini.

“Mafanikio haya ya kudhibiti biashara hii haramu ya binadamu ni kutokana na kuwepo kwa sheria ya mwaka 2008 na kanuni zake ambapo imeweza kutusaidia kudhibiti biashara hii kwa kutumia sheria za nchi,” alisema Simbachawene.

Aliongeza kuwa, mipaka ya nchi ipo imara na Serikali inaendelea kuimarisha zaidi ambapo imeweza kudhibiti watu wanaoingia na kutoka katika mipaka mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Balozi Dkt. Wright aliipongeza Tanzania inavyoshughulikia biashara haramu ya binadamu na alikiri hajawahi kukutana na kesi za ajabu zinazohusiana na biashara hiyo.

“Watanzania watu wakarimu, wastaarabu na wenye furaha wakati wote, hivyo nafurahi kuwa Tanzania kama Balozi wa Nchi hii, na Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali” alisema Balozi Dkt. Wright.

Pia Waziri Simbachawene alimuhakikishia Balozi huyo kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Marekani katika maeneo ambayo yana maslahi kwa Tanzania na Marekani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad