TUNDU Lissu, mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameeleza kukerwa na fikra za ‘ubeberu’ zinazopandwa kwake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Akijibu swali la mwandishi kwamba, anatajwa kuwa nyuma ya mabeberu kwenye harakati zake za kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lissu alianza kujibu kwa kuhoji ‘beberu ni nani?’
Akizungumza na baadhi ya wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini, nyumbani kwake Tegeta, jijini Dar es Salaam leo tarehe 9 Septemba 2020, Lissu amesema hizo ni fikra za hovyo.
“Kwanza beberu ni nani? Marekani? kama ndio hao mbona ndio wanafundisha polisi wetu, wanatoa mafunzo kwa polisi na wanaolipa ni hao hao. Mbona polisi na usalama wanafundishwa na hao?
“Mnaletewa madwa ya Ukimwi na wao? mbona hizi ni fikra za ….. hizi ni nchi rafiki tangu wa Tanzania wakati wa Nyerere (Mwl. Julius Nyerere), Mwinyi (Alhaj Ali Hassan Mwinyi), Mkapa (Hayati Benamin Mkapa), Kikwete (Dk. Jakaya Kikwete) amesema Lissu na kuongeza:-
“Tuna ujasiri wa kuwaita watu hawa mabeberu wakati tunaomba misaada kwao? nani anayesaini mikataba ya madini nao? nani anamiliki migodi ya madini ya Buliyanhulu, Nyamongo? hao mnawaita mabeberu?”
Akizungumzia kesi sita za jinai zinazomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lissu amesema mahakama zisione tabu kumsubiri amalize harakati zake za kuingia Ikulu na kisha atarejea kwenye mashitaka yake.
“Kesi zimesimama kwa miaka mitatu nikiwa nje ya nchi, na dunia inajua nilikuwa nje kwa sababu gani. Nipo kwenye kampeni za uchaguzi ambao hutokea mara moja kila baada ya miaka mitano.
“Mahakama haiwezi kunisubiri nimalize hili?” amehoji Lissu na kuongeza “nafikiri Mahakama ya Kisutu inaelewa uchaguzi huu ni muhimu kuliko hizo kesi sita, kuja kwangu nchini ni ushaidi kwamba siogopi. Tutakutana mahakamani baada ya tarehe 28 Oktoba 2020,” amesema.