Zitambue athari 5 za kukopesha Pesa na Bidhaa kwa Wateja



Katika jaamii zetu za kiafrika suala la mikopo ya bidhaa au fedha kutoka kwenye biashara kwenda kwa wateja limezoeleka sana. Ingawa jambo hili linaweza kuwa na manufaa kwa upande fulani, hata hivyo kutokana na kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watu wengi jambo hili limekuwa na athari nyingi kuliko faida.

Inawezekana umekuwa ukiwakopesha wateja wako wa maana sana, au umekuwa ukitumia mikopo kama njia ya kuuza huduma au bidhaa zako, lakini karibu nikushirikishe athari tano za mikopo hiyo.


1. Kumpoteza mteja


Kuna usemi usemao kumkopesha mteja ni kumfukuza. Nimesikia mara kadhaa wafanyabiashara wakisema tangu ni mkopeshe haji tena dukani kwangu, au tangu nimkopeshe anapita mbali tu. Mara nyingi mteja akishakopeshwa pesa au bidhaa haji tena kwenye biashara husika ili kukwepa kulipa deni. 


Kuliko umpoteze mteja kwa kumkopesha ni bora umueleze ukweli kwa kutumia busara; ingawa hatofurahi kwa wakati ule lakini baada ya muda atakuelewa na ataendelea kuwa mteja wako.


2. Ugomvi au kuharibu mahusiano


Kuna msemo usemao kukopa harusi kulipa matanga. Mara nyingi watu huja kwa uso mzuri uliojaa furaha na uaminifu wakati wa kukopa. Mara tu baada ya kukopa maisha ya shari na kusumbuana yanaweza kutokea hasa kwa wale wateja wasio waaminifu kulipa deni.


Kuna wafanyabiashara walioishia kugombana vibaya au hata kuvurugika kabisa kwa mahusiano yao na baadhi ya wateja wao kutokana na kuwakopesha bidhaa au pesa kutoka kwenye biashara zao.


Hivyo basi, kuliko uishie kugombana na wateja wako au watu wako muhimu, ni vyema ukaepuka suala hili la mikopo katika biashara yako.


3. Athari katika mzunguko wa pesa


Pesa za biashara zinatakiwa kuzunguka na si kukaa eneo moja. Mtaji wa biashara unapokuwa bidhaa katika biashara, bidhaa hizo zinapaswa kuuzwa; baada ya bidhaa hizo kuuzwa tunatakiwa kupata mauzo ambayo hujumuisha sehemu ya mtaji na faida. Mtu anapokopa pesa au bidhaa kutoka kwenye biashara yako, moja kwa moja anavuruga mzunguko huu.


Hili husababisha matatizo kama vile kukosa pesa timilifu kwa ajili ya manunuzi au gharama nyingine. Tatizo hili limewasababishia wengine kuchukua pesa zao binafsi au zilizoko nje ya biashara ili kuzipa pengo lililotokana na mikopo ili biashara isiyumbe.


4. Kupoteza fedha na mali


Kwa hakika hakuna hakikisho la asilimia mia moja kuwa pesa au bidhaa ulizomkopesha mteja zitalipwa. Ikizingatiwa kuwa watu wengi hukopeshana pesa na bidhaa kienyeji bila kufuata taratibu za kisheria zinazoweza kuwalinda baadaye iwapo mkopaji hatokuwa mwaminifu.


Hivyo basi, mikopo inaweza kukusababishia kupoteza fedha na mali ulizowakopesha wateja iwapo wateja hao hawatakuwa waaminifu kulipa, jambo ambalo linaweza kukuathiri pia kibiashara. 


5. Kufilisika au kufa kwa biashara


Hoja hii ni hitimisho tu la hoja zilizotangulia; ikiwa mikopo haitalipwa kwa wakati au haitolipwa kabisa, biashara yako inaweza kufilisika au kufa kabisa. Imeshuhudiwa wafanyabiashara wakiwa na mikopo wanayodai kutoka kwa wateja wao ambayo inazidi hata nusu ya mitaji yao; huku wakiwa hawana uhakika kama watalipwa pesa hizo au laa. Ni muhimu sana kulichukulia swala la mikopo kwa tahadhari kubwa lisije likasababisha biashara yako  kufa.


Je kuna lolote unaloweza kufanya? Ndiyo, Mueleze mteja ukweli kwa njia ambayo ni ya busara na hekima ili aelewe lengo lako. Hatakama hatokuelewa kwa wakati huo, usihofu, kadri muda unavyokwenda ataelewa hata kupitia mfanyabiashara mwingine mwenye msimamo kama wa kwako. Kumbuka uhai wa biashara yako ni muhimu kuliko mikopo ya wateja. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad