Afisa Tarafa Bashnet awakumbusha wazazi kuchangia chakula cha Mchana kwa Wanafunzi



Afisa Tarafa wa Tarafa  ya Bashnet iliyopo wilayani Babati mkoani Manyara, Glory Absalum  amewataka wazazi kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano za kuboresha maendeleo ya elimu kwa kuchangia upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni ili kuwajengea wanafunzi mazingira mazuri ya kujisomea na kushindana kimasomo.


Ameutoa Wito huo akizungumza kwenye  mahafali ya 37 ya darasa la saba katika shule ya msingi Maganjwa kata ya Dabil  yaliyofanyika katika viwanja vya Shule hiyo jana.


Amesema bila wananchi kutia nguvu katika suala la upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi, lengo la serikali la kuhakikisha kuwa inaboresha elimu kwa kila mtoto halitafikiwa, badala yake kutaibuka matabaka kwa baadhi ya Watoto kupata chakula cha mchana na wengine kukosa kabisa.


Amesema kwa kufanya hivyo, wazazi watasaidia kupunguza  changamoto za utoro shuleni, na kujenga mazingira mazuri ya Watoto kusoma ambapo mtoto akipata mlo wa mchana atapata nafasi  nzuri ya kumsikiliza mwalimu tofauti na mtoto aliye na njaa.


Glory amesema kuwa pamoja na juhudi kubwa za Serikali ya awamu ya tano ya Mhe.Rais Dkt John Pombe Magufuli kutoa elimu bure, ikiwa baadhi ya Watoto wataendelea kusoma pasipo kupata chakula cha mchana hakutawajengea mazingira sawa ya kujifunzia.


 Ameeleza kwa kinachofanywa na serikali ni kusaidia watoto wa masikini ambao hawakuwa na uwezo wa kusoma kutokana na kukosa ada hivyo ikaamua kuwekeza huko kwa kutoa fedha jambo lililosaidia ongezeko la uandikishaji watoto wanaoanza shule.


Pamoja na hayo Afisa Tarafa aliendesha harambee kwa ajili ya kumalizia madarasa matatu ya shule hiyo ambapo ilipatikana jumla ya shilingi laki 650, 000.


Mwenyekiti wa Chama cha Walimu  wilaya ya Babati  Erasto Philipo,  amesema ni muhimu serikali kuanzia ngazi ya chini ikahamasisha wazazi  kuhusu umuhimu wa watoto kupata chakula shuleni kwa kuwa inasaidia wanafunzi kupata masomo yao kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad