MMOJA wa wabunge wawili wa upinzani aliyetangazwa kushinda hadi sasa wakati mchakato wa majumuisho ya mwisho ukiendelea, Shemsia Mtamba, wa Mtwara Vijijini (CUF) aliyembwaga mmoja wa vigogo na aliyewahi kuwa waziri katika serikali kwa vipindi tofauti, Hawa Ghasia (CCM), amesema atajisikia mpweke kwa kuwa anahisi wapinzani watakuwa wachache bungeni.
“Nimefurahi sana baada ya kutangazwa kuwa mshindi, nimepambana sana katika uchaguzi huu mpaka kufikia hatua ya kutangazwa. Niliwapa sera nzuri wapiga kura wangu wakavutiwa na kunichagua. Kwa kweli sijajisikia vizuri sana kuwa mpinzani peke yangu. Nadhani kuna mambo mengi hayakwenda vizuri kwa upande wangu, nitajitahidi vizuri kuipaza sauti yangu, naamini itasikika vizuri,” amesema Shamsia.
Wakati huohuo, mchakato wa kujumuisha matokeo ukiendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hadi sasa zaidi ya majimbo 205 yameshatangazwa huku mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli, akiongoza na kuwaacha mbali wapinzani wake.
Katika majimbo yote yaliyotangazwa, mpaka sasa ni majimbo mawili tu yamechukuliwa na upinzani huku majimbo yaliyotazamwa kama ngome ya upinzani kwa miaka mingi, yakinyakuliwa na CCM.