Familia ya watu watano iliyokuwa ikiishi maeneo ya Pugu Stesheni jijini Dar es Salaam, imeteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Oktoba 14, 2020, huku uchunguzi wa awali ukionyesha kuwa chanzi cha moto huo kikitajwa kuwa ni hitilafu ya umeme.
Akizungumza hii leo baba wa familia hiyo Edward Jeremiah Katemi, amesema kuwa zoezi la kuikoa familia lilikuwa gumu kwani hata walipojaribu kulipigia simu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilishindwa kufika kutokana na adha ya usafiri iliyokuwepo siku ya jana kutokana na mvua kubwa iliyonyesha.
"Chanzo ni shoti ya umeme iliyopelekea nyumba yangu kuungua, madhara yaliyotokea ni mke wangu kipenzi, mdogo wangu pamoja na wanangu watatu wameniacha, chanzo ni umeme ulikatika tangu asubuhi, uliporudi ukakatika tena, nahisi uliporudi tena ulikuja kwa kasi zaidi", ameeleza, Katemi
"Tulijaribu kila njia ya kuwaokoa lakini ilishindikana kwa sababu tulikuwa sisi tu wananchi, tuliwasiliana na 'Fire' lakini wakashindwa kufika, baadaye tuliweza kubomoa ukuta na tukaanza kuwatoa lakini bahati mbaya walikuwa wamezidiwa na tulipowapeleka hospitali wakawa wamefariki", amesimulia baba wa familia.