KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije amemuondoa mshambuliaji wa timu hiyo, John Bocco kwenye kambi ya timu hiyo.
Stars iliingia kambini mapema wiki hii kujiandaa na mchezo wa kirafiki ulipo kwenye Kalenda ya FIFA dhidi ya Burundi uliopangwa kupigwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ndayiragije alisema kuwa katika kikosi chake Bocco pekee ndiye atakayeukosa mchezo huo dhidi ya Burundi lakini wengine wote watakuwepo.Ndayiragije alisema kuwa Bocco alipata majeraha tangu akiwa Simba ambaye aliripoti kambini na baadaye akamuondoa kutokana na tatizo hilo.
“Katika kikosi changu mchezaji ambaye atakayeukosa mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi ni Bocco pekee, lakini wengine wote wapo fiti kwa ajili ya mchezo huo.
“Hivi sasa ninaendelea na mazoezi ya pamoja kujiandaa na pambano hilo dhidi ya Burundi, ninaamini siyo mchezo mwepesi kwetu ambao ni lazima tupate matokeo mazuri,” alisema Ndayiragije na kuongeza:“Nimefurahia kuona wachezaji wangu wote wanaocheza nje ya nchi wakiripoti kwa wakati isipokuwa Himid (Mao) ambaye ana udhuru, anatarajiwa kuwasili nchini siku yoyote ndani ya siku hizi mbili.”Waandishi: Joel Thomas, Wilfred John, Julius Richard, Hadija Halifa na Karim Omary