Boss wa Maduka ya Vunjabei afunguka ishu ya Kutoka Kimapenzi na Hamissa Mobeto

 


KATIKA siku za karibuni kwenye mitandao ya kijamii, limetrend jina la Fred Vunjabei, akihusishwa kutoka na mwanamitindo, Hamisa Mobetto, ambaye ni baby-mama wa Diamond Platnumz na pia Dj Majizzo.


Mwanaspoti limepiga stori na Fred kutaka kufahamu kuhusu rais huyu wa lebo ya muziki ya Too Much Much Money inayommiliki msanii Whozu. Endelea...!


UKARIBU NA WASANII


Fred, 33, ambaye jina lake kamili ni Fred Fabian Ngajiro, ni mfanyabiashara wa mtandao wa maduka ya mavazi ambayo anasema yamechangia kumuweka karibu na wasanii na wanamichezo.


Anasema ukaribu wake na wasanii umechochewa pia na kufanya kazi nao ikiwamo kudhamini maonyesho yao na katika kutangaza mavazi yake.


ISHU YA MOBETO


 

Fred anasema Hamisa ni mtu wake wa karibu sana, lakini hana uhusiano naye wa kimapenzi.


“Marafiki wangu wa nguvu ukiwataja utaanza na Mobetto kisha utamalizia kwa Frank Knows. Sina uhusiano na Hamisa zaidi ya urafiki wa kawaida na kikazi,” anasema.


Fred anasisitiza kwamba hawezi kuwa na uhusiano na mrembo huyo kwani yeye na Diamond ni watu wanaoshirikiana kwenye biashara.


“Mimi nikiwa na Diamond tukikaa huwa tunazungumzia mambo ya biashara, hatujawahi kuzungumza kuhusu mambo yaliyo nje ya hayo,” anasema Fred ambaye anatajwa hadi kwenye nyimbo za rapa Young Lunya.


BILLNASS, YOUNG LUNYA


Fred anasema lebo yake ya Too Much Money kwa sasa inamsimamia Whozu lakini lengo lao ni kusimamia wasanii 30.


Fred anasema katika lebo hiyo yupo na wenzake wawili akiwemo kaka wa damu wa Whozu anayefahamika kwa jina la Frank Knows.


“Hii kampuni tuliianzisha China, mimi na Frank tukishirikiana na Mchina Fong Sayun na mpaka sasa tupo nayo kampuni hii.”


Aliongeza: “Pia tupo katika mazungumzo ya kuwachukua Bill Nas, Young Lunya na Odong Odwa ili kuwaongeza katika familia yetu.”


SHOO YA ZUCHU


Katika shughuli zilizofanyika hivi karibuni hakuna shaka kabisa kwamba ile shoo ya msanii wa Wasafi, Zuchu ilifana kutokana watu wengi kupendezwa na kilichofanyika.


Fred anasema katika shoo hiyo alisimamia kuwavalisha watu waliokuwa wamemzunguka Diamond na baadhi ya watu wengine.


“Diamond alikuwa amevishwa na mtu tofauti (Hamisa Mobetto) lakini mimi nilihusika kuwavalisha watu wengine waliokuwa wamemzunguka.”


Aliongeza kwa kusema; “Haikuwa jambo dogo mimi kuwa kama mfadhili mkuu katika shoo ile kwa sababu Zuchu kwa sasa ni miongoni mwa wasanii wakubwa wa kike kwenye thamani, najivunia kufanya naye kazi.”


AVISHA MASTAA


Katika kusapoti sanaa na michezo nchini, Fred hivi karibuni alimzawadia bondia staa wa taifa, Hassan Mwakinyo vocha yenye thamani ya dola 10,000 (zaidi ya Sh. 23 milioni) ya manunuzi ya nguo kwenye maduka ya Vunja Bei itakayodumu kwa muda wa mwaka mmoja.


“Kama tusingempa vocha hii angetumia pesa zake kununua mavazi kwa sababu yeye ni kijana na anahitaji kupendeza,” alisema Fred kuhusu udhamini huo wa Mwakinyo.


Bondia huyo alishukuru kwa sapoti hiyo akisisitiza kwamba: “Umaridadi huficha umasikini. Na unadhifu huongeza thamani ya mtu.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad