MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Hassan Bumbuli amefunguka kuwa kuchelewa kulipwa kwa faini yake kumetokana na kusubiri kupata barua ya hukumu yake ambayo ameipata Jumatatu ya wiki hii.
Bumbuli ametoa kauli hiyo baada kuchelewa kulipa faini ya Sh milioni tano iliyotokana na kutoa taarifa za uongo na upotoshaji katika suala la lililohusu shauri la aliyekuwa kiungo wa Yanga Mghana, Bernard Morrison ambapo alisema Yanga haijapewa nakala ya hukumu ya shauri la Morrison huku akifahamu kwamba nakala hiyo ilichukuliwa siku moja kabla.
Bumbuli amesema kuwa, katika suala hilo hawezi kukurupuka kwenda kulipa bila ya kupata barua ya hukumu ambayo ameipokea Jumatatu ya wiki hii pamoja na kujua taratibu zengine za kufanya malipo hayo kabla ya kuomba muongozo wa kufuata kwa ajili ya kufanya malipo.
“Huwezi kukurupuka kwenda kulipa, TFF wametoa hukumu na katika hukumu walisema rufaa ipo wazi lakini kuna utaratibu ndiyo unaweza kuchukua uamuzi wa kwenda kulipa au kukata rufaa, yaani huwezi kufanya kama walivyofanya wengine au huyo nani amefanya na mimi nifanye, ameambiwa faini leo, kesho ameenda kulipa kesho kitu ambacho ni kama unaitukana TFF.
“Lazima kwanza uonyeshe thamani ya wale watu waliokaa, wakakuhukumu, uonyeshe uzito wao, tulikuwa tunasubiri nakala ambayo wameileta juzi Jumatatu, nimeipata barua imewasilishwa ofisini.
“Imesomwa na tumewaandikia tena kuomba hatua kwa sababu wametuandikia nakala ya hukumu kwa hiyo watupe hatua tunalipaje, tunaenda kulipa benki au inahitajika kesho kama alivyopeleka mwenzetu ila sidhani kama ni busara kutangaza tumelipa au kwenda na vyombo vya habari kurekodiwa kuwa tumelipa na wao ndiyo watakuwa na jukumu la kusema kama Hassan amelipa ile hukumu,” alisema Bumbuli