KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mzambia Clatous Chama amecheza michezo minne mfululizo ya Ligi Kuu Bara huku akicheza nafasi mbili tofauti kwenye kikosi cha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck.
Kiungo huyo licha ya kuchezeshwa nafasi hizo, lakini ameonekana bado ni tishio baada ya kufanikiwa kufunga mabao mawili huku akipiga asisti moja kwa mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Mkongomani Chris Mugalu.
Wakati akitengeneza asisti hiyo kwenye mchezo na Biashara ya mkoani Mara, pia alifanikiwa kufunga mabao mawili katika mechi hiyo akipokea asisti za Luis Miquissone raia wa Msumbiji.Kiungo huyo, awali katika michezo ya mwanzoni.
Simba ilipocheza dhidi ya Ihefu FC (Uwanja wa Sokoine) mkoani Iringa na baadaye Mtibwa Sugar (Uwanja wa Jamhuri), Morogoro alikuwa akichezeshwa namba 10.Chama akicheza namba 10, Mghana Bernard Morrison yeye alikuwa akianza katika kikosi cha kwanza akicheza 11 kabla ya kutolewa katika kikosi cha kwanza.
Morrison aliondolewa katika kikosi cha kwanza na Mzambia, Larry Bwalya kwenye mchezo na Biashara ambaye kocha Sven alimuanzisha akicheza namba 10 iliyokuwa ikichezwa na Chama.
Kuingia kwa Bwalya katika kikosi cha kwanza ndiyo kulisababisha kumuondoa Morrison katika kikosi hicho cha kwanza huku Morrison akiingia kati ya dakika ya 65 na 70 za mchezo.
Chama hadi hivi sasa amecheza michezo miwili mfululizo ya ligi namba 11 tangu Bwalya alipoingia katika kikosi hicho cha kwanza ambaye licha ya kupelekwa pembeni ameonekana akifunga na kutengeneza mabao.
Sven hivi karibuni alisema: “Ninafurahishwa na kiwango cha Chama ambacho amekuwa akikionyesha, amecheza kwa kufuata maelekezo yangu na kufanikisha ushindi, kama akiendelea hivi basi atafika mbali ikiwemo kwenda kucheza nje ya nchi.”