KOCHA mkuu wa klabu ya Azam, Aristica Cioaba, amezikalia kooni klabu za Simba na Yanga katika vita ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2020/21, baada ya kuamua kutambulisha mifumo ya kibingwa kwenye kikosi chake.
Kabla ya michezo ya jana, Azam ilikuwa katika nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi zao 12, baada ya kushinda michezo yote minne iliyopita.Licha ya kushinda michezo yote minne iliyopita na kuongoza ligi kwa muda mrefu, lakini kikosi hicho kilikuwa kimefunga mabao matano pekee.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Azam, Zakaria Thabith ‘Zaka za Kazi’ alisema ndani ya siku tatu zilizopita, Cioaba ametambulisha program maalum kwenye mazoezi ya timu hiyo.
“Tunashukuru Mungu kwa mwanzo mzuri wa ligi ya msimu huu ambapo ukiachana na ukweli kwamba hatujapoteza mchezo mpaka sasa lakini kama timu pia hatujaruhusu bao lolote huku tukiwa na Prince Dube anayeongoza chati ya wafungaji bora.
“Licha ya mafanikio hayo kikosi chetu kimekuwa kikipata ushindi mwembamba jambo lililomfanya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, aje na programu maalum ya kuhakikisha timu inafunga mabao mengi kwa kila nafasi ambayo inapatikana ili kama itatokea tukafungwa bao basi tusipoteze mchezo kwa kuwa malengo yetu ni kutwaa ubingwa msimu huu,” alisema Thabith.