Spishi mpya ya dinosaria asiye na meno na mwenye vidole viwili pekee katika kila mkono amebainika kwenye jangwa la Gobi nchini Mongolia.
Watafiti kutoka chuo kikuu cha Edinburgh kilibaini mifupa kadhaa ya spishi hiyo waliopewa jina la Oksoko avarsan.
Kiumbe hicho chenye manyoya ambacho kinasemekana kiliishi miaka milioni 100 iliyopita, pia kilikuwa na mdomo mrefu, mkubwa.
Timu husika ilisema ufumbuzi huo unaweza kusaidia kuelezea vile wanyama wanavyopoteza vidole vya mikononi na miguuni kupitia mabadiliko ya spishi.
Walisema kwamba spishi hiyo ilipungua kidole kimoja mkononi ikilinganishwa na wanyama wa karibu nae.
Wanyama hao ambao walikua hadi urefu wa mita mbili, midomo yao ilifanana na ya kasuku.
Timu hiyo ilisema kwamba uvumbuzi wa kuwa dinosaria hao walibadilika miguu yao ya mbele kunaashiria waliweza kubadilisha lishe na maisha yao na wakaruhusu utofauti na hata kuzaliana.
"Oksoko avarsan - spishi hii inafurahisha kwasababu mifupa yao iko kamili na vile walivyohifadhiwa pamoja kunaonesha namna viumbe hao walivyokuwa wakitembea kwa makundi.
"Lakini cha muhimu zaidi, mkono wenye vidole viwili kulitufanya tuangalie mkono na miguu ya mbele ilivyobadilika katika kipindi chote cha mabadiliko ya maumbile ambako kulikuwa hakujawahi kufanyika hapo kabla".
Uchunguzi wa dinosaria hao ulijumuisha watafiti kutoka chuo cha Alberta na makumbusho ya dinosaria ya Philip J Currie nchini Canada, chuo kikuu cha Hokkaido nchini Japan na chuo cha sayansi cha Mongoli.