UONGOZI wa Yanga umesema kuwa haujamleta Kocha Mrundi, Cedric Kaze kwa ajili ya kuifunga Simba pekee, bali ni kuipa mataji mawili wanayoyashindania msimu huu wa 2020/2021.
Yanga juzi ilifikia makubaliano mazuri na Kaze aliyekuwa anafundisha Akademi ya Barcelona ya nchini Hispania tayari kwa kuja kukinoa kikosi hicho kinachowania mataji hayo ambayo ni Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Injinia Hersi Said alisema kuwa ujio wa Kaze umezingatia malengo mawili waliyojiwekea msimu huu ambayo ni lazima yatimie.
Hersi alisema kuwa malengo waliyoyaweka ni kuchukua ubingwa wa ligi na FA na siyo mchezo wao dhidi ya Simba, lengo ni kuwapa furaha na kurejesha imani iliyopotea kwa mashabiki wao baada ya kukosa mataji kwa misimu mitatu mfululizo.
Aliongeza kuwa mtaalam huyo analetwa kwa ajili ya kutengeneza kikosi imara kitakachorejesha heshima ya Yanga hapa nchini pamoja na kimataifa.
“Ifahamike kuwa hatumleti Kaze kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba tu, tuna mechi zaidi ya 33 ambayo ni ligi pamoja na Kombe la FA tutakalolishindania msimu huu.
“Nia yetu ni kutengeneza timu imara yenye ushindani kwa kila timu tutakayokutana nayo na siyo timu moja pekee, tuna malengo makubwa na kocha wetu mpya Kaze.
“Na kikubwa kilichowashawishi uongozi kwa Kaze ni uwezo wake wa kuongea lugha zaidi ya nne Kihispanyola, Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa hivyo itawasaidia wachezaji wetu wanaozungumza lugha moja tu kuwasiliana naye katika kutimiza majukumu yao uwanjani,” alisema Hersi.
Kaze tofauti na kufundisha Akademi ya Barcelona, pia aliwahi kupita kufanyakazi nchi za Ujerumani na Canada.