Mtaalamu wa Afya kutoka Wizara ya Afya Dkt.Jubilate Bernald, amesema kuwa ugonjwa wa kichaa cha Mbwa ni tofauti na magonjwa mengine ambapo mtu akishaanza kuonyesha dalili za ugonjwa huo hawezi kupata tiba.
Dkt.Jubilate Bernald amewataka watu kuchukua tahadhari mapema pale wanapokuwa wameumwa na mbwa na sio kusubiri mpaka dalili zinapoanza kuonekana.
"Ugonjwa huu ni tofauti kabisa na magonjwa mengine yoyote tunayoambiwa ukiona dalili wahi kituo cha afya, kwa sababu ugonjwa huu mtu akishaanza kuonyesha dalili hakuna tiba na moja kwa moja inakuwa anasubiria kifo" alisema Dr.Jubilate
Aidha Dkt.Jubilate amesema licha ya dalili ya ugonjwa huo kufafana na magonjwa mengi ameitaja dalili pekee ya ugonjwa huo ni wagonjwa kuogopa maji.
“Dalili ya peke yake ya kumtambua mtu mwenye ugonjwa huo zaidi huwa anaogopa maji na mwanga, ukimuekea maji anaweza akaogopa au akakimbia nakumwaga yale maji,anadhoofu, anabweka kama mbwa na wanakuwa na nguvu sana, wakorofi"alisema Dkt.Jubilate
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya Kichaa cha mbwa, ni ugonjwa ambao unaambukizwa kwa kungatwa na mbwa mwenye kichaa na ugonjwa huu si kwa binadamu bali hata wanyama , wastani wakuonyesha dalili za ugonjwa huo ni wiki mbili hadi mwezi inaweza ikazidi au chini ya hapo.