MAHAKAMA nchini Kenya, leo Oktoba 7, 2020 imewakuta na hatia washukiwa wawili y kupanga njama ya kutekeleza ugaidi na kusaidia kundi la magaidi katika shambulio la Westgate lililotokea mwaka 2013 jijini Nairobi na kusababisha vifo vya watu 67.
Mahakama hiyo pia imemwachia huru mshukiwa wa tatu, Liban Abdullahi, ambaye ni mkimbizi kutoka Somalia. Mshukiwa huyo wa tatu ambaye ni mkimbizi kutoka Somalia na ambaye kaka yake alikuwa mmoja wa washambuliaji, ameachiliwa huru.
Liban Abdullahi ana kitambulisho cha Kenya na ameondelewa shitaka la kuwa nchini Kenya kinyume cha sheria. Serikali imesema wanamgambo wanne waliotekeleza shambulizi hilo walipatikana wakiwa wamefariki dunia kwenye vifusi vya jengo hilo.
Zaidi ya watu 140 walitoa ushahidi kwenye kesi hiyo. Aidha washukiwa walikanusha madai ya njama ya kutekeleza ugaidi. Hakimu ametoa uamuzi kwamba washukiwa wawili wote raia wa Kenya, watahukumiwa Oktoba 22.
Mwandishi wa BBC, Ferdinand Omondi, mjini Nairobi amesema kuwa hukumu yao itakuwa inasubiriwa katika nchi ambayo bado iko katika hali ya tahadhari kuu ya uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi ya al-Shabab.
Kundi hilo lenye kuhusishwa na kundi la al-Qaeda, lina makao yake nchini Somalia na limetekeleza mashambulizi kadhaa nchini Kenya. Kenya ina wanajeshi nchini Somalia kusaidia kukabiliana na wanamgambo hao.