Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro ameelezea hali ya kisiasa nchini imeendelea kuimarika hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu na wananchi wengi wamekuwa watulivu licha ya kuwepo kwa baadhi ya watu wachache walioandaliwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa kwa ajili ya kufanya vurugu na kujiingiza kwenye uhalifu.
IGP Sirro aliyasema hayo jana jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuwataka baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kufanya masuala ya siasa na kuacha kuwatumia vijana na kuwaingiza kwenye uhalifu.
Hata hivyo, IGP Sirro alisema kuwa, yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria huku akiwataka wananchi kuepuka vishawishi vya kujiingiza kwenye uhalifu na kubeba matatizo ya wengine kwa kupata shida kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wasiowatakia mema na kushindwa kutimiza ndoto zao, alisema .
Aidha, Kuhusu upigaji wa kura Zanzibar, IGP Sirro alisema, wapo baadhi ya watu wanaohamasisha baadhi ya watu au kikundi cha watu kuvunja sheria wakati wa zoezi la upigaji kura kinyume cha sheria, kanuni na taratibu zilizopo na kwamba zoezi la upigaji kura litafanyika kwa mujibu wa tarehe iliyopangwa na litafanyika kwa amani na utulivu na kuwapata viongozi watakaowataka.