JPM: Watanzania Tuiombee Kenya Corona Itokomee



Rais Dkt. Magufuli ambaye pia ni mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) amewaomba Watanzania kutumia siku tatu kuanzia leo kumuomba Mungu virusi vya corona viondoke nchini Kenya.


 


Dkt. Magufuli amesema hayo wakati akianza kuhutubia maelfu ya wananchi waliokusanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa kampeni zake za kuomba kura kwa wananchi.


 


Amesema kabla hajafika uwanjani hapo amezungumza na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye amemwambia kuwa Wakenya watafanya maombi kwa siku tatu kuanzia leo ili COVID19 iishe nchini humo kama ambavyo imeisha nchini Tanzania.


 


Kutokana na kusudio hilo, Dkt. Magufuli amewaomba Watanzania kuungana na Wakenya katika maombi yao, na kwamba anaamini Mungu atajibu kama alivyojibu kwa upande wa Tanzania.


 


“Kabla sijaja hapa, leo asubuhi nilikuwa naongea na Rais mwenzangu wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema wameamua kufanya maombi kwa siku tatu kuanzia leo mpaka Jumapili ili kumuomba Mungu corona iondoke, na sisi tuungane nao kuwaombea corona iondoke nchini humo.” amesema Magufuli.

Shughuli mbalimbali nchini Tanzania zinaendelea kawaida baada ya serikali kueleza kuwa hakuna maambukizi ya virusi hivyo ambavyo vimeendelea kuzisumbua nchi nyingi duniani.


Hadi Oktoba 9, 2020, visa zaidi ya 40,000 vimeripotiwa nchini Kenya, ambapo kati hivyo, watu zaidi ya 26,300 wamepona huku waliofariki wakiwa ni 751.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad