KARIBU katika ‘KIPINDI MAALUM’ kutoka Global Radio, ambapo mwanasiasa Mkongwe, David Kafulila, anazungumzia masuala mbalimbalu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakaofanyika Oktoba 28, pomoja na ajenda ya vijana katika kipindi hiki cha uchaguzi.
“Mambo ambayo yatakwenda kuamriwa Ikulu, Bungeni na mabaraza ya madiwani yatakuwa ni wastani wa maamuzi ya wananchi, kwa kuwa tulipashwa tuwe tunaamua wenyewe, kutokana na uhalisia ndio maana tukaenda kwenye mfumo wa demokrasia ya uwakilishi kupitia uchaguzi.
“Kuna nchi ambazo zimekuwa zikiingia kwenye uchaguzi na baada ya uchaguzi nchi inasambaratika, hii inatokana na vijana kutumiwa vibaya, vijana tutambue kuwa tuna kesho nyingi zaidi kuliko wazee wetu, hivyo tushiriki uchaguzi huu kwa amani tusije kuua ndoto zetu.
“Mwaka 1990 Vietnam ilikuwa na uchumi wa dola bil. 6.5, Tanzania bil. 4.5 na Kenya bil. 8.4, leo Vietnam imetuacha mbali, ina bil 300, Kenya bil. 90. Vietnam alifanya nini? Alijikita kwenye kuanzisha viwanda na kuongeza uzalishaji, uwekezaji, ajira na biashara.
“Ili uwe na viwanda na vyenye tija na kuvutia wawekezaji lazima uwe na umeme wa kutosha, ndicho Serikali ya sasa inachokifanya, ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha mgao wa umeme wa mwaka 2005 pekee uliisababishia nchi kupoteza mapato ya dola bilioni 2 (TZS tril 4.6).
“Ongezeko la upatikanaji wa umeme kutoka 35% hadi 85% ni mapinduzi makubwa sana. Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2012 walikuwa wamekadiria kwamba Tanzania ingesambaza umeme nchi nzima mpaka mwaka 2100, lakini Rais Magufuli amefanya hii kazi kwa kasi sana.
“Kama Magufuli ameweza kusambaza umeme kwa asilimia 50 ndani ya miaka mitano (tukatoka 35% hadi 85%), atashindwaje kusambaza umeme kuyafikia maeneo ambayo ni asilimia 15 tu yamebaki, hesabu iko wazi na hilo linawezekana.
“Tanzania ndio inaongoza kwa kuwa na bei ndogo ya umeme Afrika Mashariki, kwa wastani ni dola senti 10 (Tsh 230) kwa unit moja, Kenya dola senti 21, Uganda senti 18, Rwanda senti 26, unaweza kuona tofauti. Tuna serikali ambayo inaendeshwa kiufanisi sana.
“Rais Magufuli alikataa kuifunga nchi sababu ya Corona, tumeona maisha ambavyo yamekuwa magumu kwa upande wa wenzetu Kenya baada ya kujifungia, Magufuli aliruhusua na watu wakalipwa mishahara, leo Dunia inatangaza Tanzania ndiyo nchi pekee haina Corona Duniani.
“Chadema katika Ilani yao wameeleza kuwa wataboresha miundombinu kwa kuweka rehani rasilimali za nchi kama madini, tafiti zinaonyesha mfumo huo ni wa rushwa na kifisadi.
“Nilisikia wanasema mkataba wa Kampuni ya Madini ya Twiga na Barrick haukupitishwa bungeni kujadiliwa, mikataba inatakiwa kuwa wazi lakini haijadiliwi Bungeni, Bunge likishiriki kujadili mikataba mbele ya safari kukawa na mapungufu litashindwa kuisimamia serikali.
“Hakuna nchi duniani iliwahi kuwa nzima ikakatwa vipande kurahisisha utawala na maendeleo, nchi unazoziona za majimbo zilikuwa hivyo tangu zikitawaliwa na wakoloni, Malaysia, DRC, Sudan Kusini, Marekani, siri ya Marekani kufanikiwa si majimbo, sababu yanaongeza gharama.
“Tanzania alishaiunganisha Mwl. Nyerere, hatuwezi kurudi tulikotoka, miundo hii ya utawala inatokana na Historia, ufumbuzi wa nchi kubwa si kukata vipande vipande ni kuchagua Rais mwenye akili kubwa ya kuiongoza hiyo nchi, wenye akili ndogo watawaza kugawanya tu.
“Ukubwa wa Jimbo la Alaska la Marekani ni karibu mara mbili ya nchi ya Tanzania, kwa nini hawajaligawa tena vipande, hili suala la majimbo linaongeza tamaa ya kuipasua nchi. Dar es Salaam inatoa kodi asilimia 60 ya nchi nzima, ukiweka majimbo huko kwingine kutakuwaje.
“DRC Jimbo la Katanga wanatamani kujitenga kila siku kwa sababu wana madini mengi ili wakale peke yao. Dar ingetamani ijitenge sababu ya ina bahari, kimsingi hakuna ushahidi kwamba majimbo yanapunguza umaskini, kwa nini Congo na Sudan ni maskini zaidi,” amesema Kafulila.