RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema upatikanaji wa viwanja kwa ajili ya kukuza soka vilivyopo Kigamboni jijini Dar na mkoani Tanga, ni miongoni mwa mafanikio makubwa kwao.
Karia alitoa kauli hiyo kwenye hafl a iliyoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) iliyofanyika jana Jumamosi jijini Dar, ambapo alisema hayo kwao ni mafanikio ya uongozi wake ndani ya miaka minne tangu aingie madarakani.
“Moja ya mafanikio ambayo yapo katika soka hapa nchini kwenye uongozi wangu ni viwanja vya Kigamboni na Tanga kupatikana hati kwa muda wa miezi miwili pamoja na hati ya ujenzi ambayo imepatikana ndani ya wiki moja jambo ambalo lilikuwa gumu kwa hapo awali.
“Pia utawala wangu ni bora katika kuhakikisha tunaondoa migogoro kisoka, usimamizi wa fedha kwa usahihi ambapo tunacheza ngoma ambayo Serikali inacheza,” alisema Karia.Karia aliongeza kuwa, mafanikio ya soka katika kipindi cha utawala wake huu, yapo mengi ikiwemo timu za soka za taifa za Tanzania kutwaa mataji mbalimbali.