Nahodha wa klabu ya Simba, John Bocco amewaomba radhi viongozi na wanachama wa mabingwa hao wa ligi kuu Tanzania bara kwa matokeo mabaya waliyoyapata katika mechi mbili mfululizo zilizopita.
Bocco ameandika kupitia mitandao yake ya kijamii amesema wanafahamu namna viongozi na wanachama wanavyoiunga mkono katika kila nyanja na wanaumizwa kwa matokeo hayo.
Nahodha huyo ambaye jana alikosa mkwaju wa penati dhidi ya Ruvu Shooting ambao walipoteza kwa kipigo cha bao 1-0, amewaahidi viongozi na wanachama kwamba watajituma maradufu ili waanze kushinda michezo ijayo.
''Wanachama viongozi pamoja na wapenzi wote wa Simba Sc, kwanza nimshukuru Mungu kwa kuwapa moyo wa upendo wana Simba wote kwa kuipenda timu yetu na kuiunga mkono katika vipindi tofauti na kila mkoa tunaokwenda kucheza.
Kwa niaba ya wachezaji niseme tunaomba mtusamehe kwa matokeo tuliyopata ya michezo yote miwili iliyopita, tuliteleza na tumeshateleza hatupaswi kuteleza tena na hii ndio ahadi yetu kwenu kurekebisha makosa yetu na kurudi wenye sura mpya na upambanaji mpya kwa michezo yote ijayo ili turudishe furaha yetu kwakupata motokeo mazuri kama tulivozoea tumesha waangusha tunakiri hili ila tunaamini hali hii haitajitokeza tena kwa michezo ijayo ,nguvu moja.''John Bocco.
Simba ipo katika nafasi ya nne katika ligi kuu wakiwa na alama 13 baada ya kushuka mara 7 uwanjani wakiwa wamepoteza mara 2 na sare moja kiasi cha kuzua hofu miongoni mwa wanachama wao kwamba huenda wakashindwa kutetea taji walilolitwaa msimu uliopita.