Kaze Amtaja Carlinhos Tatizo Yanga SC



KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, ameanza na safu ya ushambuliaji katika program zake za mazoezi ili kuhakikisha anapunguza ukame wa mabao huku akisema kina Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ ndiyo wanashindwa kuwapa pasi washambuliaji.

Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kuiona safu hiyo inayoongozwa na Mghana, Michael Sarpong, Yacouba Songne, Waziri Junior na Tuisila Kisinda.

Safu hiyo ya ushambuliaji ya Yanga hadi hivi sasa imefanikiwa kufunga mabao saba pekee huku ikiruhusu bao moja baada ya kucheza michezo mitano tangu kuanza kwa ligi.

Akizungumza na Championi Jumatano, Kaze alisema kuwa anaamini uwezo wa washambuliaji wake hao aliowakuta huku akitaja tatizo linalosababisha washindwe kufunga mabao.

Kaze alisema kuwa washambuliaji hao wameshindwa kuonyesha umahiri wao katika kufunga mabao kutokana na viungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima, Feisal Salum, Mukoko Tonombe na Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ kukosa mbinu za pamoja kuwapigia pasi za mwisho za kufunga mabao.

“Tangu nikiwa nchini Canada nilikuwa nalijua tatizo lililopo katika timu ambalo ni safu ya ushambuliaji kushindwa kufunga mabao, tatizo ambalo ninaamini nitalifanyia kazi kwa haraka ili kuhakikisha wanafunga.

“Washambuliaji akina Sarpong na Yacouba, wameonekana kushindwa kufunga mabao kutokana na viungo wao kushindwa kutimiza majukumu yao vizuri, ikiwemo kuwapa mipira mizuri ya kufunga mabao.

“Hivyo nimeanza kuiboresha safu hiyo ya ushambuliaji kwa kuhakikisha natengeneza muunganiko mzuri wa viungo na washambuliaji ambao kabla ya kuja kwangu haukuwepo,” alisema Kaze.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad