Kaze Atangaza Hali ya Hatari Yanga



MARA baada ya kutua nchini, kocha mkuu mpya wa Yanga Mrundi Cedric Kaze ameahidi kuipambania timu hiyo kwa kuhakikisha anacheza michezo iliyobakia ya Ligi Kuu Bara kama fainali na kuipa ubingwa huo kwenye msimu huu.


 


Kauli hiyo aliitoa juzi saa 10:22 usiku mara baada ya kutua nchini kwa ndege ya Shirika la Kilimanjaro Airlines akitokea nchini Canada kabla ya kubadili ndege Amsterdam, Uholanzi.




Kocha huyo anajiunga na Yanga akichukua nafasi ya Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyesitishiwa mkataba wa kuendelea kukinoa kikosi hicho ambacho kimeweka kambi yake Kijiji cha Avic Town kilichokuwepo Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar Akizungumza na Championi Jumamosi, Kaze alisema kuwa amepanga kuifanyia makubwa klabu hiyo kubwa Afrika na duniani kwa kuanza atahakikisha anauchukua ubingwa wa ligi unaotetea na watani wao Simba waliochukua mara tatu mfululizo.


 


Kaze alisema kuwa, ana matumaini makubwa ya kuuchukua ubingwa kutokana na vinara waliokuwepo kileleni Azam FC 18 na wao 13 wakiwa na mchezo mmoja mkononi wa ligi ambao kama wakishinda mchezo ujao watabakisha pointi mbili pekee, hivyo hana hofu na wapinzani wao hao katika mbio ya ubingwa.




Mrundi huyo ambaye jana alisaini mkataba miaka miwili ya kukinoa kikosi hicho, alisema kuwa kwa hivi sasa hawafikirii kabisa watani wao, Simba na badala yake nguvu na akili amezielekeza kwa kila timu atakayokutana nayo kwa kuhakikisha anashinda kila mchezo utakaokuwepo mbele yao.


 


“Mimi siwezi kufanya maandalizi ya kikosi changu kwa kwa ajili ya Simba pekee na badala yake ninafanya maandalizi kwa kila timu nitakayokutana nayo katika michezo inayofuatia ya ligi.


 


“Hivyo kila mchezo kwangu ni fainali na tutapambana kama fainali bila ya kuidharau timu yoyote, kikubwa mashabiki waondoe hofu kwenye mbio za ubingwa ligi, licha ya Azam kuwepo kileleni wakituongoza ambao nao wapo mbele kwa mchezo mmoja.




“Malengo yangu niliyokuja nayo ni kuipa ubingwa ambayo nimepanga kuyatimiza katika msimu huu, uzuri ninawafahamu na kuwafuatilia wachezaji wote tangu nikiwa Canada nilikuwa nikiwasiliana na kocha msaidizi Mwambusi (Juma) nikimpa program za mazoezi.


 


“Niwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa ndani ya muda mfupi nikiwa na kikosi changu wataona mabadiliko makubwa ikiwemo timu kucheza soka safi la kuvutia na kuelewana.


 


“Keshokutwa (leo) ndiyo ninatarajia kuanza kazi rasmi ya kuifundisha Yanga baada ya kufanya kikao na viongozi wangu na kusaini mkataba wa kuifundisha Yanga,” alisema Kaze.




AMPONGEZA KRMPOTIC


“Kocha aliyepita ameweza kupata alama 13 katika michezo 5 hakika amefanya kazi kubwa sana. Nakuja kuendeleza alipoishia. Falsafa yangu napenda timu icheze kwa kumiliki mpira mbali na goli langu, hii itamfanya mpinzani wangu kuchoka.


 


“Nataka timu yangu icheze kwa kwenda mbele na kwa malengo, sitotaka mpira wa shoo, mchezaji kapiga kanzu, sawa lakini je baada ya kanzu nini faida yake.”


 


APEWA NDINGA


Aidha, kocha huyo mara baada ya kutua alikabidhiwa gari mpya aina ya Toyota Rav 4 na wadhamini wa timu hiyo, Kampuni hiyo GSM ambayo atakuwa anaitumia kwenye mizunguko yake binafsi ya kazi kwa kipindi chote atakachokuwepo Yanga.


“Kocha mara baada ya kusaini mkataba alikabidhiwa gari jipya kabisa aina Toyota RAV 4 ambayo amepewa na GSM atakayoitumia kwa kipindi chote atakachokuwepo Yanga,” kilisema chanzo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad