Kikongwe Miaka 76 Awafanyia Kitu mbaya Wezi wa Ng’ombe!



VIJANA watano waliotuhumiwa kuiba ng’ombe 30 wa mzee Malunde Mwigulu (76), mkazi wa Kijiji cha Imalilo Kata ya Ntobo mkoani Tabora, wamelazimika kulipa ng’ombe 40 baada ya mzee huyo kuwaeleza kila aliyenunua na kula ng’ombe wake hatabaki salama.


 


Hatua hiyo imekuja baada ya vijana hao kukamatwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora na kukiri kuiba ng’ombe hao.


 


Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kwa masikitiko katika kituo cha Polisi Wilaya ya Igunga, Malunde kuwa, alisema ng’ombe wake walikuwa kambini kwa ajili ya malisho, lakini baadaye alipotembelea katika kambi hiyo iliyoko kijijini hapo, alibaini katika kundi la ng’ombe hao, 30 hawapo.


 


Alisema kuwa, baada ya kuona hali hiyo alianza kufuatilia ndipo akapata fununu kutoka kwa wasiri wake ambao hakupenda kuwataja majina waliomweleza kuwa ng’ombe hao waliibwa na kijana mmoja, Mbogo Mihayo (34) ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Tawi la Isugilo Kata ya Igunga mjini.


 


Aliongeza kuwa, baada ya fununu hiyo alikwenda kituo cha Polisi ambako alifungua kesi na kumuomba Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga, Ally Mkalipa amsaidie ili ng’ombe wake waweze kurudi.


 


“Niliwaambia ng’ombe wangu wote wakirudi sitaki kesi iende mahakamani kwani umri wangu umekwenda,” alisema mzee huyo huku akibubujikwa na machozi.


 


Alisema kuwa, baada ya siku chache alipata taarifa kutoka Polisi kuwa, washitakiwa watano tayari wamekamatwa na alipofi ka kituoni aliwakuta watuhumiwa hao Mbogo Mihayo (34), Masudi Ally (29), Yusuph Mihayo (29), Ndende Mihayo (46) na Omary Ramadhani almaarufu Gwai (39) ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa nyama.


 


Alisema; “Nilipomuuliza Mbogo kuhusu ng’ombe wangu 30, alikiri kuwa kweli yeye ndiye aliyeiba huku akisema kuwa tayari amekwishawauza kwa wafanyabiashara wanne ambapo alimuomba mzee huyo waelewane ili aweze kumlipa.


 


Mkuu wa Polisi Wilaya ya Igunga, Ally Mkalipa alisema licha ya kwamba yeye siyo msemaji wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, lakini anachojua ni kwamba huyo mzee aliibiwa ng’ombe 30.


 


Mkalipa alisema watuhumiwa wote walikubali kulipa ng’ombe 40 Oktoba 15, 2020 ambapo ng’ombe 10 ni kama fi dia ya gharama aliyopata mzee huyo ambapo watuhumiwa wote wapo nje kwa dhamana.


 


Akizungumza kwa niaba ya watuhumiwa wenzake, mfanyabiashara maarufu wa nyama, Omary Ramadhani (Gwai) alisema kuwa, yeye binafsi alinunua ng’ombe saba kihalali, lakini amekubali baada ya mzee huyo kusema kuwa kila aliyenunua ng’ombe na aliyekula hatabaki salama.


 


“Sisi tumeamua kulipa ng’ombe kwa kiasi kila mmoja alichonunua kwani tumepata taarifa huyu mzee ni mganga wa kienyeji hivyo tumeogopa kupoteza maisha yetu,” alisema Gwai.


 


Nao baadhi ya wananchi, Samson Idd, Sululu Selemani, Elizabeth Leonard wamelipongeza Jeshi la Polisi Igunga kwa kufanikiwa kumuokoa mali za mzee huyo.


 


“Tunamshukuru mzee huyu kwa kuacha kutumia uganga wake vibaya kwani angepoteza maisha ya watu wengi wa maeneo mbalimbali ya walionunua kitoweo hicho,” alisema mmojawao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad