HATIMAYE kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi ndiye ataisimamia timu hiyo kwenye mechi ya Simba na Yanga Agosti 18.
Yanga, juzi ilitangaza kuvunja mkataba wa aliyekuwa kocha wao Zlatko Krimpotic na haikusema kocha mpya wa timu hiyo atakuwa nani, lakini Championi limepenyezewa kuwa Mwambusi amepewa kazi ya kuisimamia timu hiyo kwa mechi tatu na kama akifanya vizuri basi atabaki hapo hadi dirisha dogo ndiyo watatafuta kocha mwingine.
Kati ya makocha ambao Yanga wamewaweka kwenye listi ya kuchukua nafasi ya Mwambusi kama atachemka ni George Lwandamina raia wa Zambia, Kaze Cedric raia wa Burundi au Mjerumani Ernst Middendorp.
“Kwa sasa Mwambusi ndiye kocha mpya wa timu na ataisimamia kwenye michezo mitatu, kama akishindwa kufanya vizuri basi tutatafuta kocha mwingine.lakini akifanya vizuri tutaenda naye hadi dirisha dogo ndiyo tutafute kocha mwingine lakini tunaamini kuwa anaweza kufanya kazi nzuri.
Lakini kuna makocha watatu wanaweza kuchukua nafasi yake ambao ni Lwandamina, Cedric na raia wa Ujerumani.
Lwandamina ana historia nzuri na Yanga baada ya kufanikiwa kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara moja msimu wa 2016-2017. Lakini nafasi ya pili ni Cedric mwenye historia nzuri kwenye soka la Afrika anatajwa kuwa ni mtaalam wa mpira wa chini na wa pasi fupifupi na hana masihara.
Mrundi huyo amefanya kazi nchini Canada na ndipo alipokaa kwa muda mrefu, akiwa amefundisha timu ya Atletico ya Burundi na kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Gazeti hili jana lilimtafuta kocha huyo raia wa Ujerumani ambapo alisema:“Bado hakuna jipya sana, nasikia kuna mtu anaitwa Senzo (Mazingiza), amekuja kunifuata hilo mimi sijui, lakini subiri hadi Jumanne nitakupa jibu ya nini kinaendelea,” alijibu kocha huyo mwenye rekodi nzuri ameshafundisha soka kwenye mabara matatu, Asia, Afrika na Ulaya
Mbali na Kaizer kocha huyo Mjerumani amewahi kuzifundisha, Asante Kotoko, Heat of Oak za Ghana, Chippa United, Martizburg, Celtcs na Golden Arow za Afrika Kusini.
Anatajwa kuwa kati ya makocha wenye heshima kubwa sana kwenye soka la Afrika Kusini kutokana na kufanikiwa kufundisha timu nyingi kubwa za nchi hiyo.