Dar es Salaam. Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Kanda ya Dar es Salaam- Temeke imeiamuru kampuni ya Quality Group Limited kuwalipa waandishi wake wa habari wa zamani 23 iliowaachisha kazi mwaka 2017, jumla ya Sh232,324,172.96 (zaidi ya Sh232 milioni).
Tume hiyo inayofanya kazi kama Mahakama ya Mwanzo ya Migogoro ya Kazi, iliiamuru kampuni hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu Yusufu Manji, kuwalipa waandishi hao kiasi hicho cha pesa, baada ya kuridhika kuwa ilivunja mikataba baina yao kwa kuwaachisha kazi bila sababu maalumu.
Ilifikia uamuzi huo baada ya wanahabari hao kufungua shauri la mgogoro wa kikazi, wakipinga uamuzi wa kampuni hiyo kuwaachisha kazi kabla ya muda wa mikataba yao w miaka miwili waliyosainiana kuisha.
Wanahabari hao walikuwa wakifanya kazi katika gazeti la JamboLeo, lililokuwa likimilikiwa na kampuni ya Manji ya Quality Media Ltd, ambapo waliachishwa huku mlalamikiwa akitoa sababu kwamba alikuwa amesikia mambo mazuri kuwahusu wao.
Katika shauri hilo, wanahabari hao, Joseph Lugendo na wenzake 22 walidai kuwa waliajiriwa na mdaiwa huyo kwa nyakati tofauti kwa mikataba ya miaka miwili, lakini Septemba 19, 2017 hata kabla muda wa mikataba yao haujaisha, mdaiwa aliwaachisha kazi.
Hivyo, pamoja na mambo mengine walikuwa wakiiomba tume hiyo iiamuru kampuni hiyo iwalipe fidia kwa uvunjai wa mkataba kabla ya muda na malipo ya mishahara ya miezi iliyokuwa imesalia kabla ya mikataba yao kufikia mwisho.
Pia walikuwa wakidai nyongeza ya mishahara kulingana na makubaliano ya kimkataba, cheti cha huduma, fidia ya madhara ya jumla, malipo ya mishahara hadi tarehe ya uamuzi wa shauri hilo na ujira maalumu (kamisheni).
CMA katika tuzo (uamuzi) alioutoa Juni 24, mwaka jana, Msuluhishi aliyefahamika kwa jina la Kokusiima L, amekubalina na madai na maelezo ya ushahidi wa walalamikaji hao kuwa kilichofanywa na mlalamikiwa ni uvunjaji mkataba kwani hakuzingatia sheria.
Alisema kuwa hapakuwa na sababu halali ya usitishaji wa mikataba ya walalamikaji kabla ya muda kuisha. Aliongeza kuwa sababu aliyoitoa mlalamikiwa ni kinyume cha kifungu cha 8(1) (d) cha Kanuni za Ajira na Mahusiano Kazini (Kanuni za Utendaji Bora) za mwaka 2007.
Msuluhishi alifafanua kuwa sababu aliyoitoa kwamba amesikia kitu kizuri kutoka kwa wafanyakazi wenzao ni tata, kwani hakuna namna ambavyo mtu anaweza akaachishwa kazi kwa kusikia habari nzuri kuhusu yeye. Kwa mujibu wa CMA, mlalamikiwa hakuzingatia sheria ambayo inataka kutoa taarifa ya siku zisizopungua 28.
Hata hivyo, Msuluhishi Kokusiima alisema kwa kuwa mikataba ya walalamikaji ilikuwa ni ya muda maalumu, basi kanuni ya kuachishwa kazi kusiko kwa haki haiwezi kutumika na kwamba walalamikaji wana haki ya kulipwa mishahara ya miezi ilioyokuwa imebakia tu.
“Kwa hiyo katika kesi hii, kushindwa kwa mlalamikiwa kuzingatia masharti ya mkataba hususan kifungu cha muda wa usitishaji mkataba, anawajibika kumlipa kila mlalamikaji mishahara kwa miezi iliyokuwa imebakia ya mkataba wa ajira,” alisema Msuluhishi na kuongeza:
“Mdaiwa anawajibika kuwalipa walalamikaji (wote kwa ujumla) jumla ya Sh232,324,172.96. Pia kila mlalamikaji sharti apewe hati cheti safi cha huduma. Walalamikaji walishindwa kuthibitisha madai mengine hivyo yanatupiliwa mbali.”