Jaji wa mahakama kuu nchini Uganda Musa Sekaana ametupilia mbali ombi la wanachama wa zamani wa chama cha NURP Difas Basile na Hassan Twaha waliomshitaki Robert Kyagulanyi na viongozi wengine wa chama cha NUP kwa kubadili jina la chama chao kinyume na sheria na walipe gharama za kesi.
Mosese Kibalama Nkonge aliyekuwa rais wa chama NURP na katibu wake mkuu Paul Nsimbwa walikubali kukabidhi chama na kubadilisha jina la chama hicho na kuitwa NUP na kumuchagua Robert Kyagulanyi kuwa kiongozi mpya wa chama hicho.
Kyagulanyi ametumia chama chake kipya cha NUP kwenye kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2021, na kulikuwa na wasiwasi kwamba kama mahakama ingerudisha chama hicho kwa jina la zamani Bobi Wine na wagombea wake wa ubunge na udiwani wangekuwa wagombea wa kujitegemea wasio na chama.
Aidha, katika hotuba yake na wandishi wa habari Bobi Wine amesema kuwa sasa anakwenda kuteuliwa Novemba 3, 2020 na tume ya uchaguzi kugombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 dhidi ya rais aliyekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 30 Yoweri Museveni.