Majaliwa: Tukamchague Dkt. Magufuli Tumemjaribu Na Ameweza



JUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema ni muhimu kwa Watanzania wakatumia busara kwa kumchagua mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili aendelee kuliletea Taifa maendeleo kwa kuwa kazi ya urais si ya kumpa mtu ambaye hajawaji kujaribiwa na kuonesha kuwa anauwezo wa kuongoza. 


“Rais Dkt John Pombe Magufuli ndiye mgombea mwenye sifa thabiti za kuliongoza Taifa hili na katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake ameweza kuwatumikia Watanzania kwa uaminifu mkubwa na mnajua ni kwa namna gani ambavyo ametuletea maendeleo watu wote bila kujali vyama, makabila na uwezo wetu.”


Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Oktoba 10, 2020) alipozungumza na wananchi wa Kata ya Daluni wilayani Mkinga, Tanga katika mkutano wa kampeni ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt. Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Mkinga, Dastan Kitandula na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM


Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Magufuli amefanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii nchini ikiwa ni pamoja utoaji elimumsingi bila ada na kuwawezesha watoto wa Kitanzania kusoma bure na bila ya ubaguzi wowote. Pia ameboresha huduma za afya na kuwawezesha wananchi kutibiwa karibu na makazi yao. “Maendeleo hayana chama tukamchague Dkt. Magufuli ni mchapakazi.”


Amesema kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Serikali itaendelea kuboresha zaidi utoaji wa huduma za kijamii nchini, hivyo amewaomba Watanzania wahakikishe ifikapo Oktoba 28 mwaka huu wajitokeze kwa wingi na kwenda kuwachagua wagombea wa CCM katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani.


Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imekamisha taratibu za kuwagawia wananchi shamba la Mwele lililoko wilayani Mkinga ili waweze kulitumia kwa ajili ya shughuli za kilimo, baada ya shamba hilo kuachwa kwa muda mrefu bila ya kuendelezwa. Hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.


Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema mashamba matano ya mkonge yanayomilikiwa na Bodi ya Mkonge pamoja na mashamba mengine ambayo hayajaendelezwa Serikali


imeagiza yagawiwe kwa wananchi walime mkonge ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi wa kipato.


Amesema katika kipindi cha miaka mitano (2015/2016 – 2019/2020) sambamba na kuimarisha uzalishaji wa zao la mkonge ikiwa ni sehemu ya mazao ya kimkakati ya biashara Serikali imeweza kurejesha mali mbalimbali za Serikali zilizouzwa kinyume na utaratibu ikiwemo nyumba za makazi zaidi ya 30.


Mheshimiwa Majaliwa amezitaja mali nyingine zilizorejeshwa kuwa ni pamoja na jengo la Makao Makuu ya Bodi ya Mkonge Tanzania, maghala, hisa na fedha taslim (USD 78,000 na Shilingi milioni 34) zilizokuwa zimehifadhiwa zaidi ya miaka 20 kwenye akaunti ya mfilisi (Liquidator) bila ya kuwasilishwa Serikalini.


Amesema hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kuimarisha mfumo wa kilimo cha mkonge kwa wakulima wadogo nchini ambapo katika mwaka 2019/2020 idadi yao iliongezeka na kufikia 7,551 ikilinganishwa na wakulima 5,828 wa mwaka 2015/2016 na itaendelea kufufua na kuendeleza mashamba yaliyokuwa yametekelezwa yakiwemo Marungu Sisal Estate (Tanga mjini) Kwamgwe Sisal Estate (Handeni).


 

Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa mkonge nchini na kutoa ajira kwa wananchi wengi hususani kwa vijana na hivyo kuongeza mapato ya Serikali ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM. “Mwitikio wa wananchi wa wilaya ya Mkinga  ni mkubwa katika kufufua zao la mkonge.”



 


 (mwisho)   


IMETOLEWA:


JUMAMOSI, OKTOBA 10, 2020. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad